Breaking News

MAONESHO YA NNE YA SEKTA YA DAWA, MATIBABU NA AFYA KUFANYIKA DAR ES SALAAM

Maonesho maalum ya nne ya biashara kwenye sekta ya dawa, huduma za afya na matibabu yanatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 21 hadi 23 Agosti 2025 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

Taarifa kutoka waandaaji wa maonesho hayo zinaeleza kuwa zaidi ya makampuni 80 kutoka nchi tano za Afrika Mashariki yatashiriki, huku yakileta pamoja Pharmatech & Health East Africa pamoja na Medical & Lab East Africa.

Zaidi ya wageni 2,500 kutoka Tanzania na mataifa jirani wanatarajiwa kuhudhuria, wakiwemo wadau wa afya, wazalishaji wa dawa, wahudumu wa maabara na wataalamu wa fani mbalimbali.

Katika maonesho hayo, bidhaa na huduma mbalimbali zitaonyeshwa zikiwemo dawa, vifaa vya matibabu, teknolojia za maabara, vifaa vya upasuaji, bidhaa za meno na za mifupa. Pia mada kuhusu utalii wa tiba, matibabu asilia na tiba za Ayush zitajadiliwa, kwa lengo la kuboresha huduma za afya nchini.

Maonesho hayo yatakuwa wazi kwa wananchi bila kiingilio, na wageni watapata nafasi ya kushiriki katika majukwaa ya mijadala, mafunzo na mikutano mbalimbali.

Tukio hilo linaandaliwa na ETSIPL kwa kushirikiana na Chama cha Wadaktari wa Dawa Tanzania, kwa msaada wa Wizara ya Afya, TMDA, MEWATA, na Chama cha Madaktari wa Mifupa Tanzania (TOA). Pia limeungwa mkono na TANTRADE na kufadhiliwa na wadau wakuu akiwemo MSD, AENON Health Care, Planet Pharmaceutical Ltd, na NCD.

Kwa mujibu wa waandaaji, maonesho hayo yatatoa fursa kubwa ya kubadilishana maarifa, kujifunza teknolojia mpya na kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya afya.

Wananchi na wadau wa sekta ya afya wanakaribishwa kutembelea maonesho hayo kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni katika siku zote tatu.