Breaking News

WAUMINI WA MSIKITI WA ISLAAH KIGOGO WAMUOMBA RAIS SAMIA KUINGILIA MGOGORO NA MWEKEZAJI

Katibu wa Kamati ya Waumini, Bw. Abdulraheem Swaliyah akizunguzia mgogoro huo kwa niaba ya Waumini wa Msikiti wa Islaah uliopo Kigogo, jijini Dar es Salaam.

Wazee mbalimbali wa msikiti wa Islaah uliopo Kigogo jijini Dar es Salaam wakiwa katika mkutano huo na waandishi wa habari.


Dar es salaam - Waumini wa Msikiti wa Islaah uliopo Kigogo, jijini Dar es Salaam, wamemwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati mgogoro wa muda mrefu kati yao na mwekezaji.

Akizungumza kwa niaba ya waumini Agosti 16, 2025, Katibu wa Kamati ya Waumini, Bw. Abdulraheem Swaliyah, alisema chanzo cha mgogoro huo ni kitendo cha mwekezaji kutaka kuhamisha umiliki wa msikiti kutoka mikononi mwa waumini na kuupeleka chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).

“Mara baada ya kuingia makubaliano ya kufungua shule, mwekezaji alianza kufanya vitendo vinavyokiuka makubaliano, ikiwemo mchakato wa kubadili umiliki wa msikiti kinyume na tulivyokubaliana,” alisema Bw. Swaliyah.

Alifafanua kuwa licha ya jitihada mbalimbali kufanyika kutafuta suluhu, ikiwemo kumshirikisha Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Walid Alhad Omar, mwekezaji huyo amekuwa akikosa ushirikiano.

Aidha, alisema kwa mujibu wa katiba ya msikiti huo, baadhi ya viongozi waliopo tayari wamepoteza sifa za kuendelea kushika nafasi hizo, na sasa wako madarakani kwa mpito wakisubiri uchaguzi wa viongozi wapya.

“Hata hivyo, kila mara tunapomuarifu mwekezaji kuhusu uchaguzi, amekuwa akikwepa kutoa ushirikiano, jambo ambalo limekuwa kikwazo kikubwa kwa waumini kupata viongozi halali kwa mujibu wa katiba yetu,” aliongeza Bw. Swaliyah.

Waumini hao wamesema wameona ni vema kumwomba Rais Samia kuingilia kati ili kumaliza mgogoro huo unaodaiwa kudumu kwa muda mrefu bila kupata ufumbuzi.