MASAUNI AJIVUNIA MAFANIKIO YA JIMBO LA KIKWAJUNI, AWATAJA RAIS SAMIA NA RAIS MWINYI
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Zanzibar na mtia nia wa ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amewashukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi, kwa utekelezaji mkubwa wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020, uliosaidia kusukuma mbele maendeleo ya Jimbo la Kikwajuni na taifa kwa ujumla.
Akizungumza Agosti 19, 2025 wakati wa kutoa tathmini ya utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja na ahadi zake jimboni humo, Mhe. Masauni alisema kasi kubwa ya maendeleo imeonekana katika sekta mbalimbali za kijamii, ikiwemo ongezeko la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama pamoja na fursa za ajira kwa vijana.
“Nichukue fursa hii kuwashukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na vilevile Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanikisha. Kwa sasa changamoto nyingi katika Jimbo langu la Kikwajuni zimepungua,” alisema Masauni.
Aidha, aliwashukuru wananchi wa Kikwajuni kwa ushirikiano waliompa wakati wa kipindi chake cha ubunge, akibainisha kuwa mshikamanon huo umekuwa chachu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo.