Breaking News

RAIS SAMIA AONGEZA VIWANDA 671 SIMIYU NDANI YA MIAKA MINNE

Mkoa wa Simiyu umefanikiwa kuongeza viwanda 671 ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, hatua iliyotokana na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji.

Takwimu zinaonesha idadi ya viwanda imeongezeka kutoka 671 mwaka 2020 hadi 1,342 mwaka 2025. Kati ya hivyo, viwanda vikubwa vimeongezeka kutoka 8 hadi 15, vya kati kutoka 4 hadi 10 na vidogo kutoka 660 hadi 1,317.

Miongoni mwa viwanda vikubwa vilivyofunguliwa ni pamoja na kiwanda cha kuzalisha mabomba ya plastiki cha Kampuni ya Moil kilichopo Wilaya ya Bariadi chenye uwezo wa kuzalisha mabomba 1,300 kwa siku na kuajiri wafanyakazi 422, kati yao 102 wa kudumu.

Vingine ni kiwanda cha kuchambua pamba cha Rajencro Agro Industry LTD kilichopo Maswa chenye uwezo wa kuchokota kilo 350,000 za pamba kwa siku na kutoa ajira 132, pamoja na kiwanda cha Bio Sustain Tanzania LTD cha Meatu chenye uwezo wa kuchakata kilo 500,000 za pamba kwa siku.

Aidha, Kampuni ya TRIWAN Tanzania LTD imejenga kiwanda cha kuchakata mafuta ya alizeti na pamba wilayani Bariadi chenye uwezo wa kuchakata tani 400 za mafuta ya alizeti na tani 600 za pumba kwa siku. Pia, kiwanda cha BigOne Company LTD kilichopo Maswa kina uwezo wa kuchambua tani 150 za pamba kwa siku.

Chama Kikuu cha Ushirika Simiyu (SIMCU) pia kimefufua kiwanda cha kuchambua pamba kwa gharama ya shilingi bilioni 4 chenye uwezo wa kuchambua zaidi ya tani 400 za pamba kwa siku. Vilevile, Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imekamilisha ujenzi wa kiwanda cha kimkakati cha kutengeneza chaki kwa gharama ya shilingi bilioni 8.09 ambacho kitaweza kuzalisha katoni 174,000 za chaki kwa mwaka na kutoa ajira zaidi ya 340 pindi kitakapoanza uzalishaji kamili.

Kwa upande mwingine, serikali inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuzalisha nyuzi za pamba katika Wilaya ya Itilima ambapo eneo la ekari 1,000 linatarajiwa kutwaliwa kwa ajili ya mradi huo.

Matokeo ya ongezeko la viwanda hayo yamechangia kuimarika kwa ajira kutoka 3,701 mwaka 2020 hadi 7,037 mwaka 2025, ikiwemo ajira za kudumu 2,408 na za muda 4,629.