MGOMBEA UBUNGE TEMEKE KUPITIA CHAMA CHA AAFP AAHIDI MAENDELEO
Na Neema Mpaka, Dar es Salaam – Mgombea Ubunge wa Jimbo la Temeke kupitia Chama Cha Wakulima (AAFP), Yusuph Rai, amesema endapo wananchi watampa dhamana ya kuliongoza jimbo hilo, atahakikisha Temeke linapiga hatua kubwa za kimaendeleo na kuwa tofauti na majimbo mengine ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Rai alitoa kauli hiyo leo mara baada ya kuchukua fomu ya uteuzi wa kugombea ubunge katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Bi. Fortunata Shija.
Akizungumza na waandishi wa habari, Rai alisema kuwa licha ya Dar es Salaam kuwa na barabara nyingi na vituo vya afya vya mfano, Jimbo la Temeke limekuwa likibaki nyuma kimaendeleo.
“Uhalisia wa sasa unaonyesha Temeke ni kama dampo ukilinganisha na majimbo mengine ya Dar es Salaam kama Kinondoni, Ilala, Kawe na Kibamba,” alisema Rai.
Aidha, alibainisha kuwa Temeke lina rasilimali nyingi ikiwemo uwepo wa viwanda, kampuni, wafanyabiashara wakubwa, pamoja na miundombinu ya kitaifa kama Uwanja wa Taifa na Maonesho ya Sabasaba, hivyo wananchi wa jimbo hilo wanapaswa kunufaika moja kwa moja na fursa hizo.
“Tukipeleka mbunge wa kariba kama yangu, nitahakikisha vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na makundi mengine wanapata fursa za maendeleo. Pia nitashirikiana na wawekezaji kuhakikisha wanawaangalia wananchi wa Temeke wanapowekeza,” alisisitiza.
Rai alisema endapo atateuliwa rasmi kuwania ubunge, ataanza kampeni zake kwa kuwafikia wananchi katika kata zote 13 na mitaa yote ya Temeke, akisisitiza kuwa hatakuwa mgombea wa matusi bali atawasilisha Ilani ya AAFP na mikakati ya maendeleo.
“Nataka Watanzania wajue kwa nini makao makuu ya chama chetu yapo Temeke. Tupo tayari kupambana usiku na mchana kuhakikisha mwaka huu Temeke inapata mbunge mwenye kiu ya kutatua kero za wananchi,” alisema