Breaking News

MGOMBEA UBUNGE MBAGALA KIPITIA CHAMA CHA AAFP AAHIDI KUSHUGULIKIA KERO ZA WANANCHI

Na Neema Mpaka, Dar es Salaam - Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mbagala kupitia Chama Cha Wakulima (AAFP), Ndonge Said Ndonge, ameahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo endapo atapewa ridhaa ya kuwa mbunge wao katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea Ubunge kutoka kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bi. Fortunata Shija, Ndonge alisema moja ya kero kubwa ni mradi wa ujenzi wa fremu za biashara zinazodaiwa kujengwa kwenye hifadhi ya barabara ya mradi wa mabasi yaendayo haraka (Mwendo Kasi) katika eneo la Chamazi–Kongowe.

Amedai kuwa fremu hizo zimejengwa kinyume cha taratibu za kisheria, na licha ya kuathiri miundombinu muhimu ikiwemo mfereji wa majitaka na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Serikali imeshindwa kumchukulia hatua mwekezaji husika.

> “Mimi ni mwananchi wa kawaida, nazifahamu shida zote za Mbagala. Nimeamua kugombea kwa sababu hakuna mwingine atakayetatua matatizo haya. Wananchi tusibaki kusubiri viongozi waliopo, tuchague sisi wenyewe,” alisema Ndonge.

Kuhusu mradi wa Mwendo Kasi, Ndonge alibainisha kuwa nauli zinazotajwa kuwa juu kuliko daladala hazina uhalali kwa kuwa mradi huo umefadhiliwa kwa sehemu na Benki ya Dunia huku wananchi wakiendelea kulipa kodi.

> “Haiwezekani daladala kutoka Mbagala hadi Kariakoo iwe shilingi 600, halafu Mwendo Kasi utulazimishe kulipa shilingi 1,000 au 1,500. Serikali lazima ihakikishe nauli za Mwendo Kasi zinakuwa nafuu kuliko daladala,” alisisitiza.

Aidha, aligusia changamoto za miundombinu ya barabara na biashara ndogo ndogo, akilalamikia ubaguzi katika utekelezaji wa sheria ambapo wafanyabiashara wadogo wanafukuzwa mitaani, huku mwekezaji anayepangisha fremu katika eneo la Mwendo Kasi akiachwa bila kuchukuliwa hatua.

“Haiwezekani mtu akijenga barabarani na kupangisha fremu akachukuliwa kama halali, wakati mfanyabiashara mdogo akiweka biashara barabarani anafukuzwa. Wananchi wa Mbagala lazima tushikamane kutafuta haki yetu, kwa sababu hakuna kiongozi mwingine atakayekuja kututatulia matatizo,” alisema.

Ndonge alihitimisha kwa kusisitiza kuwa malengo yake ni kuhakikisha wananchi wa Mbagala wanapata huduma bora, usawa katika utekelezaji wa sheria na maisha bora kupitia miundombinu rafiki na usafiri nafuu.