Breaking News

MIKOPO YA ASILIMIA 10% YAFIKIA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 227.96 MWAKA 2024

Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imefanikisha ongezeko kubwa la mikopo kwa makundi maalumu ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu kupitia utekelezaji wa agizo la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2020 mikopo iliyotolewa kwa vikundi 32,553 ilifikia shilingi bilioni 93.3 pekee. Hata hivyo, ifikapo mwaka 2024 kiasi hicho kimeongezeka mara dufu na kufikia zaidi ya shilingi bilioni 227.96, sawa na ongezeko la shilingi bilioni 134.

Ongezeko hilo limechangiwa na usimamizi bora wa marejesho na ufuatiliaji thabiti wa utekelezaji wa sera hiyo. Hatua hii imeongeza fursa za ajira, kukuza mitaji ya wajasiriamali wadogo na kuongeza kipato cha wananchi moja kwa moja.

Kwa mujibu wa Wizara husika, utekelezaji endelevu wa mpango huo unaendelea kutoa mchango mkubwa katika kupunguza umasikini na kuongeza ushiriki wa makundi maalumu katika uchumi wa taifa.