Breaking News

NGOME YA CHAUMA SEGEREA YABOMOKA, WANACHAMA 200 WAREJEA CHADEMA

Dar es salaam - Zaidi ya wanachama 200 wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) katika Jimbo la Segerea, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, wamekihama chama hicho na kurejea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wakieleza kutoridhishwa na mwenendo wa uongozi ndani ya chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Agosti 25, 2025, kwa niaba ya wanachama hao, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHAUMA Kata ya Kinyerezi, Mndewa Mndewa maarufu kwa jina la Dk. Timo, alisema wameamua kuondoka kutokana na mifumo mibovu ya uongozi isiyo ya kikatiba.

“Tumegundua mifumo ya uongozi ndani ya CHAUMA siyo ya kikatiba, bali chama kipo kwa maslahi binafsi ya baadhi ya watu,” alisema Dk. Timo.

Aidha, aliwataka wananchi wa Segerea kutokuwa wepesi wa kuingia katika uchaguzi mkuu kwa mihemko ya kisiasa na kufuata wagombea wa vyama visivyo na mizizi madhubuti.

Awali akizungumzia mgombea ubunge wa CHAUMA katika Jimbo hilo, Dk. Timo alisema: “Huyu anayetaka kugombea Segerea kwa tiketi ya CHAUMA aliwahi kuwa mbunge kwa miaka mitano. Anakuja leo na sera ya mikopo. Miaka yote mitano iliyopita mliwahi kumwona hapa Segerea?”

Aliwaonya wananchi wawe makini na ahadi zinazotolewa na baadhi ya wagombea wa upinzani, hususan zile zinazodai mikopo ya vikundi kutolewa ndani ya miezi mitatu baada ya uchaguzi.

“Huu ni uhuni wa kisiasa. Anakuja kuwadanganya wananchi waunde vikundi ili awape mikopo baada ya uchaguzi, jambo ambalo haliwezekani,” alisisitiza.

Kwa upande wake, aliyekuwa Ofisa Habari wa CHAUMA Kata ya Kinyerezi, Salumu Nasoro, alisema ameamua kurejea CHADEMA kutokana na mfumo mbovu wa kiutendaji ndani ya chama hicho.

Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa CHAUMA Kata ya Bonyokwa, Mohammed Mussa, alisema ameamua kubwaga manyanga na kurejea CHADEMA baada ya kuchoshwa na mwenendo wa chama hicho.

Aidha Dk. Timo aliwataka viongozi wa CHAUMA Segerea kuwa watulivu, akibainisha kuwa endapo wakijaribu kupotosha ukweli, atafichua mapungufu makubwa ambayo yataitikisa ngome nzima ya chama hicho katika jimbo hilo.