TUCTA YAZINDUA JENGO JIPYA ARUSHA, JOWUTA YAPOKELEWA RASMI
Na Mwandishi Wetu, Arusha - Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limezindua rasmi jengo jipya la biashara jijini Arusha, hafla iliyokwenda sambamba na kukabidhi vyeti kwa vyama vyake wanachama.
Miongoni mwa vyama vilivyopokea vyeti ni Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA). Cheti hicho kilikabidhiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, kwa Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma Siwayombe.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, alisema kujiunga kwa JOWUTA kunafanya idadi ya vyama wanachama kufikia 16 kutoka 13 vya awali. Alisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia wanahabari kupata fursa mbalimbali ikiwemo kutetewa maslahi yao na kupatiwa elimu ya masuala ya kazi.
Vyama vingine vipya vilivyopokea vyeti ni Chama cha Wafanyakazi Sekta ya Ulinzi Binafsi (TUPSE) na Chama cha Wafanyakazi wa Huduma za Viwandani Tanzania (TASIWU).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JOWUTA, Musa Juma, aliishukuru TUCTA kwa kuwapokea na kuahidi kuwa kipaumbele cha chama hicho ni kutetea maslahi na mazingira bora ya kazi kwa wanahabari.
“Tutashirikiana na viongozi wengine wa TUCTA kuhakikisha wanahabari wanafanyakazi kwa kuzingatia sheria, wakiwa na ajira na mikataba inayotambulika kisheria,” alisema.
Naye Waziri Ridhiwani aliwataka wafanyakazi kuendelea kushirikiana na serikali akisema shirikisho hilo lina historia kubwa nchini kabla na baada ya uhuru.
“Ambaye haoni umuhimu wa shirikisho hili, huyo si mzalendo. Serikali haiwezi kusahau mchango wa wafanyakazi katika mafanikio ya sekta mbalimbali ikiwemo elimu, ujenzi wa SGR na maendeleo ya bandari,” alisema.
Jengo jipya la TUCTA
Akieleza kuhusu jengo jipya lililozinduliwa, Waziri Ridhiwani alisema ni uthibitisho wa mchango wa vyama hivyo katika uchumi na maendeleo ya kijamii, kwani mbali na kuisaidia TUCTA pia litachangia ukusanyaji wa kodi.
Awali, Rais wa TUCTA Nyamhokya alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza mwaka 1975, na baadaye ukaendelea mwaka 2023 ambapo umekamilika kwa asilimia 98. Jengo hilo lina jumla ya wapangaji 113 na linatarajiwa kuingizia shirikisho mapato ya Sh milioni 50 kwa mwezi.
“Mbali na vyumba vya biashara, jengo lina hoteli na chumba maalum cha wageni (Presidential Suite),” alisema Nyamhokya.