Breaking News

WANANCHI CHANGAMKIENI FURSA YA BIMA - TIRA

Wananchi jijini Arusha wametakiwa kujitokeza kwa wingi kutembelea banda la Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Themi Njiro, ili kupata elimu ya kina kuhusu umuhimu wa bima kwenye maisha ya kila siku na shughuli za kiuchumi.

Meneja wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Bahati Ogolla, amesema mamlaka hiyo imeshiriki kwenye maonesho hayo kwa lengo la kuwafikia wananchi moja kwa moja, hususani wakulima, wafugaji na wavuvi, ili kuwapa uelewa wa huduma za bima na namna zinavyoweza kuwa ngao dhidi ya majanga.

Amesema kupitia maonesho hayo, wananchi wanaweza kukutana na watoa huduma wa sekta hiyo na kupata maelezo kuhusu aina mbalimbali za bima, ikiwemo bima za kilimo, mifugo na uvuvi.
“Bima ni kinga dhidi ya majanga Ikitokea janga, kampuni ya bima inatoa fidia kulingana na makubaliano ya mkataba, hii inasaidia wananchi kuepuka hasara kubwa na kurudi haraka kwenye shughuli zao za uzalishaji,” amesema Ogolla.

Amefafanua kuwa bima hugawanyika katika makundi mawili bima ya muda mrefu au bima ya maisha inayodumu zaidi ya mwaka mmoja, na bima ya muda mfupi isiyozidi mwaka mmoja, ikiwemo bima za magari, moto, meli, ndege, wizi, dhima na ajali.

Kwa upande wa kilimo, amewataka wakulima kutumia fursa ya bima ya kilimo inayolinda mazao dhidi ya majanga kama ukame au mafuriko.

“Nawaomba wananchi, hasa wakulima, wafike kwenye banda letu wapate elimu. Bima ina manufaa makubwa, inasaidia kufidia hasara, na pia inaweza kuwa chanzo cha ajira kupitia uwakala wa bima,” amesisitiza.