Breaking News

WATUMISHI WA SUA WATEMBELEA HIFADHI YA NGORONGORO KUUNGA MKONO UTALII WA NDANI

Ngorongoro – Baadhi ya watumishi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametembelea Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro ikiwa ni sehemu ya ziara yao ya kujifunza na kuunga mkono juhudi za kuhamasisha utalii wa ndani.

Ziara hiyo ilihusisha kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuangalia mandhari ya kipekee na wanyamapori adimu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, mmoja wa washiriki alisema kuwa matembezi hayo yamewapa fursa ya kufahamu kwa undani urithi wa nchi na kuongeza ari ya kushiriki katika kulinda na kutangaza vivutio vya utalii wa Tanzania.

Uongozi wa Ngorongoro pia uliwahimiza watumishi hao kuendelea kuwa mabalozi wa hifadhi na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika utalii wa ndani, ambao ni sehemu ya kukuza uchumi wa taifa.