Breaking News

WAWAMI KUTOA ELIMU JUU YA MMOMONYOKO WA MAADILI, AMANI, UMOJA NA MSHIKAMANO

Dar es Salaam - Asasi isiyo ya kiserikali ya Wazee wa Mtaani na Wazee Watarajiwa (WAWAMI) imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa jamii kwa lengo la kuhamasisha amani, mshikamano na upendo kuanzia ngazi ya familia, ili kusaidia kutokomeza mmomonyoko wa maadili nchini.

Akizungumza makao makuu ya asasi hiyo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa WAWAMI, Bw. Khamis Iddi Kituga, alisema taasisi hiyo imejikita katika kutoa elimu kupitia semina, vipeperushi na vyombo vya habari ili kuchochea ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa taifa.

“Tukiwa kama wazee wastaafu, tumedhamiria kutoa elimu kwa jamii, hususan vijana, juu ya masuala mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha wanakua na ustawi mzuri sambamba na kutambua mila na desturi zetu, ili kuepusha mmomonyoko wa maadili,” alisema Bw. Kituga.

Alibainisha kuwa WAWAMI imepanga kuandaa mikutano ya kijamii, semina pamoja na vikao maalum na watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili kuwapa elimu ya maadili na kuwakumbusha umuhimu wa mila na desturi za Kitanzania.

Aidha, alisema kupitia mikutano hiyo, vijana watafundishwa kujitambua, kujiandaa na maisha ya uzeeni, huku wakipata uzoefu na ujuzi kutoka kwa wazee.

“Tunataka jamii iwe na maarifa ya kuwa walinzi wa mila na desturi, washauri na wapatanishi, ili hatimaye waweze kuwa wazazi bora wa baadaye,” aliongeza.

Mbali na hayo, asasi hiyo pia imepanga kusaidia kutafuta fursa za kielimu kwa wenye vigezo, wakiwemo watoto wanaoishi katika mazingira magumu na waliopitia changamoto za kifamilia au kifungo, pamoja na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani kila Oktoba Mosi.