Breaking News

BRELA YAIMARISHA UWAZI WA KIBIASHARA KWA KUTEKELEZA SHERIA YA WAMILIKI MANUFAA

Dar es Salaam – Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umechukua hatua thabiti kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika sekta ya biashara nchini, kwa kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Umiliki Manufaa wa Kampuni na majina ya biashara. Hatua hii inalenga kudhibiti vitendo vya uhalifu wa kifedha, ikiwemo utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Makampuni na Majina ya Biashara wa BRELA, bwana Isdori Nkindi, hatua hizo ni utekelezaji wa Pendekezo Na. 24 la Kundi Kazi la Kimataifa la Kupambana na Uhalifu wa Kifedha (FATF), linalotaka nchi wanachama kuhakikisha taarifa sahihi za wamiliki halisi wa kampuni zinapatikana kwa urahisi kwa taasisi husika.
“Kila nchi mshirika wa FATF inapaswa kuhakikisha taasisi zake zote zinazohusika na mapambano ya uhalifu wa kifedha zinaelewa vyema namna ya kufikia taarifa sahihi za umiliki manufaa, ili kuzuia uhalifu kabla haujatokea,” amesema Nkindi.

Mafunzo na ushirikiano wa kitaasisi

Tangu mwaka 2023, BRELA imeendesha mafunzo kwa taasisi mbalimbali ikiwemo TAKUKURU, Jeshi la Polisi, TRA, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Uhamiaji, Mahakama na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali. Mafunzo hayo yalilenga kuongeza uelewa wa namna taarifa za wamiliki manufaa zinavyoweza kusaidia kufuatilia na kudhibiti uhalifu wa kifedha.
Aidha, elimu hiyo imetolewa kwa mawakili, taasisi binafsi, wafanyabiashara na wamiliki wa kampuni wa ngazi zote, kwa lengo la kuhakikisha wanakidhi matakwa ya Sheria ya Kampuni Sura ya 212 na Kanuni za Umiliki Manufaa za mwaka 2023.

Haki, uwazi na bunifu

Katika utekelezaji wake, BRELA pia imeweka mkazo kwenye umuhimu wa uwazi katika taarifa za usajili, hatua ambayo inaleta uwanja sawa kwa wafanyabiashara na kuongeza imani kwa wawekezaji. Kanzidata ya kitaifa ya usajili wa makampuni na majina ya biashara inatazamiwa kuwa nyenzo muhimu ya haki kibiashara na ubunifu, kwa kuwa inarahisisha upatikanaji wa taarifa kwa taasisi za uchunguzi na wananchi.

Wito kwa vyombo vya habari

Nkindi amesisitiza kwamba vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kufikisha elimu hii kwa wananchi ili wajue wajibu wao na kuepuka kukiuka sheria.

“Tunashirikiana na wadau wote, lakini pia tunaendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kudhibiti na kuwasaka wanaovunja sheria hii,” amesisitiza na kiongeza kuwa

"Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2020 na marekebisho ya mwaka 2023 yameweka msingi wa utekelezaji wa dhana ya wamiliki manufaa nchini. Kupitia elimu, ushirikiano wa kitaasisi na ufuatiliaji wa karibu, BRELA inaonesha dhamira ya kuimarisha uwazi, haki na ubunifu katika mazingira ya biashara ya Tanzania