DKT. SAMIA AAHIDI MAENDELEO YA KILIMO, MAJI NA MIUNDOMBINU TUKUYU, MBARALI NA NJOMBE
Mbeya, Njombe – Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na ziara yake ya kampeni Nyanda za Juu Kusini, akipokelewa kwa shangwe kubwa na maelfu ya wananchi katika mikutano ya hadhara Tukuyu, Mbarali na Njombe Mjini.
TUKUYU: Katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Tukuyu, Dkt. Samia aliambatana na viongozi mbalimbali wa kitaifa wa CCM akiwemo Katibu Mkuu, Dkt. Asha-Rose Migiro na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Kenan Kihongosi.
Akiwahutubia wananchi, Dkt. Samia alisema dhamira ya CCM ni kuhakikisha kila kijiji na kitongoji kinapata huduma bora za msingi ikiwemo maji, umeme, shule na vituo vya afya.
Akijikita zaidi kwenye kilimo, alizungumzia changamoto za sekta ya chai na parachichi. Kuhusu chai, alisema mashamba yaliyokabidhiwa kwa wawekezaji binafsi yatafanyiwa tathmini ili kuhakikisha yanawanufaisha wakulima kupitia vyama vya ushirika. Aidha, aliwataka wawekezaji waliopo kulipa madeni yao kwa wakulima na wafanyakazi kabla ya serikali kuchukua hatua
Kuhusu parachichi, alisema Tanzania inashika nafasi ya tatu barani Afrika kwa uzalishaji, lakini kushuka kwa bei kumeathiri wakulima. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, serikali imepanga kujenga vituo 50 vya kuhifadhia parachichi na mbogamboga, viwili kati ya hivyo vikiwa Rungwe. Pia, kupitia mpango wa kongani za viwanda na programu ya BBT, serikali itajenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na kuendelea kutoa ruzuku ya pembejeo ili kuongeza tija.
MBARALI: Katika mkutano wa pili uliofanyika Mbarali, Dkt. Samia alikumbusha wananchi juu ya miradi iliyotekelezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, maji na miundombinu.
Alisema hospitali moja ya wilaya, vituo vya afya vinne na zahanati tisa zimejengwa, sambamba na shule mpya 35 za msingi na 14 za sekondari. Pia, miradi mikubwa ya maji yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 51.5 inatekelezwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Katika sekta ya umeme, alibainisha kuwa kati ya vitongoji 712 vya Mbarali, tayari 641 vimeunganishwa na huduma hiyo na ameahidi kukamilisha vilivyosalia. Zaidi ya shilingi bilioni 11 zimetumika kuboresha barabara na madaraja kupitia TARURA, huku zaidi ya kilomita 464 za barabara za changarawe zikiboreshwa.
Dkt. Samia pia alisisitiza umuhimu wa kulinda Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa kuhamisha vijiji vilivyopo ndani yake, kwani ndiyo chanzo cha maji yanayozalisha umeme kwenye mabwawa ya Mtera na Kidatu. Aliahidi fidia kwa wananchi walioathiriwa na mchakato huo.
NJOMBE MJINI: Akiendelea na ziara yake, Dkt. Samia alihitimisha siku yake kwa mkutano mkubwa mjini Njombe. Alikumbusha wananchi kuhusu maboresho ya huduma za afya ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe na kuongeza vituo vya afya 13.
Katika sekta ya elimu, alisema shule mpya 62 za msingi na 48 za sekondari zimejengwa, huku barabara kuu kadhaa zikikamilika ikiwemo Njombe–Makete (km 107.4) na Njombe–Moronga (km 53.9). Mtandao wa barabara za lami umeongezeka kutoka kilomita 274 mwaka 2020 hadi kilomita 468 mwaka 2025.
Aidha, aliahidi kuendelea na ujenzi wa barabara muhimu zinazounganisha Njombe na mikoa jirani, ikiwemo Itone–Ludewa–Manda na Makete–Isonje–Mbeya.
Kuhusu nishati, Dkt. Samia alisema mradi wa kuzalisha umeme wa Mto Ruhuji (358 MW) unaendelea, na wananchi wanaodai fidia watalipwa kwa mujibu wa sheria. Katika maji, aliahidi kukamilisha miradi ili kufanikisha mpango wa “kumtoa mama ndoo kichwani.”
Sekta ya viwanda nayo imeshuhudia ongezeko la viwanda vikubwa kutoka 8 hadi 17, huku kongani za viwanda zikitarajiwa kuanzishwa katika kila wilaya. Katika kilimo, ruzuku ya mbolea imeongezeka kutoka tani 57,950 mwaka 2020 hadi tani 97,585 mwaka 2025, na wakulima walionufaika wameongezeka kwa zaidi ya 40,000.
Dkt. Samia pia aliahidi kufufua viwanda vya chai, kujenga vituo vya kuhifadhia parachichi na kuharakisha ujenzi wa uwanja wa ndege wa Njombe ili kuongeza biashara na usafirishaji wa mazao. Alisema miradi mikubwa ya Liganga na Mchuchuma ipo katika hatua za mwisho kabla ya kuanza utekelezaji, hatua itakayoongeza ajira kwa vijana.