Breaking News

CHUMI: AFRIKA KUPATIWA FEDHA ZA MABADILIKO YA TABIANCHI NI ISHARA YA USAWA KATIKA MAJUKUMU YA KIMATAIFA NA SI MSAADA WA HURUMA

Addis Ababa, Ethiopia - Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi amesisitiza kuwa si sawa kwa Afrika kushurutisha nchi zilizoendelea kutoa fedha za mabadiliko ya tabianchi, kwani ni wajibu wao wa msingi katika kulinda tabianchi duniani kote.

Mhe. Chumi ameyasema hayo akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango katika Mjadala uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Afrika kuhusu Tabianchi Addis Ababa, Ethiopia ukiangazia Mahitaji ya Fedha ya Afrika ya Ufadhili wa Mabadiliko ya Tabianchi Kabla ya COP30 (Africa’s Climate Finance Demands Ahead of COP30).
“Afrika haitakaa tena pembeni na kungoja. Tunapiga hatua mbele kudai nafasi yetu stahiki katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ulimwenguni. Bara letu linastahili ufadhili wa uhakika, wa haki na wa kutosha ili kufikia suluhu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kupunguza athari zake, na kuendeleza maendeleo stahimilivu kwa Afrika. Hili si suala la hisani,” amesisitiza Naibu Waziri Chumi.

Ameeleza kuwa ufinyu wa fedha ni moja ya changamoto kubwa zinazozuia kupiga hatua kubwa katika mapambano hayo. Afrika ambayo inachangia 4% tu katika uchafuzi wa hali ya hewa, inahitaji dola bilioni 61 kila mwaka kugharamia mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo kwa sasa inapokea kiasi cha chini ya 36% ya fedha hizo. Mhe. Chumi ameongeza kuwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara hupokea chini ya 5% ya fedha hizo na ndio waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi ukilinganisha na uchangiaji wake katika janga hilo.
Mjadala huo umewaleta pamoja Naibu Waziri Chumi, Waziri wa Misitu, Uvuvi na Mazingira wa Afrika Kusini Mhe. Dkt. Dion George, Mjumbe Maalum wa COP30 anayeiwakilisha Afrika, Bw. Carlos Lopes, na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hasara na Uharibifu, Bw. Ibrahima Diong ambapo wamejadili umuhimu wa kufanyika kwa mageuzi ya mifumo ya kimataifa ya fedha ili iwe rafiki kwa nchi zinazoendelea katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, Viongozi hao wametoa wito wa kuchukua jitihada jumuishi baina ya Afrika na nchi zilizoendelea kuhakikisha upatikanaji wa dola za kimarekani trilioni 1.3 kila mwaka kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hadi kufikia 2035 ‘A New Collective Quantified Goal’. Wameisifu na kuunga mkono mifumo ya fedha za tabianchi zinazoakisi hali ya Afrika na kupambaniwa na Afrika.