SHEIKH JALALA AONGOZA MATEMBEZI YA MAULID, AAMASISHA UPENDO NA MSHIKAMANO
Dar es Salaam — Kiongozi Mkuu wa Waislamu wa Jumuiya ya Shia Ithna’ashariyyah Tanzania (T.I.C), Sheikh Jalala, leo ameongoza matembezi ya amani ya Maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W.W), yaliyoanzia Kigogo Roundabout na kumalizika katika viwanja vya Pipo, Kigogo Post.
Akihutubia mamia ya waumini waliojitokeza kushiriki, Sheikh Jalala amewataka Waislamu nchini kuenzi na kuishi kwa vitendo mafunzo ya Mtume Muhammad (S.A.W.W).
“Leo tumefanya matembezi haya ya amani kusherekea mazazi ya Mtume. Ni vyema kama taifa tuendelee kuyaenzi na kuyaishi yale aliyofundisha na kuyaishi katika kipindi chote cha uhai wake,” alisema Sheikh Jalala.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa mshikamano miongoni mwa Waislamu wa madhehebu yote, akibainisha kuwa Mtume Muhammad (S.A.W.W) alihimiza umoja, upendo na mshikano bila kujali tofauti za kiitikadi.
Katika wito wake kwa Watanzania, Sheikh Jalala amewaasa kuendelea kulinda tunu za taifa la amani, mshikamano na upendo, hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
“Nitoe wito kwa Watanzania kuendelea kulinda amani na mshikamano tulionao. Mwenyezi Mungu amlinde Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wake ili waendelee kuongoza kwa hekima na busara,” aliongeza Sheikh Jalala.
Maadhimisho ya Maulid mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo: “Mtume wa Amani: Uchaguzi Uwe wa Haki, Demokrasia na Amani.”