DOYO AAHIDI BARABARA ZA KIWANGO CHA JUU SERENGETI
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Mheshimiwa Doyo Hassan Doyo, ameahidi kuipa kipaumbele Wilaya ya Serengeti katika miradi ya barabara na miundombinu endapo atachaguliwa kuunda serikali ijayo.
Akihutubia wakazi wa Mji wa Mugumu wakati wa ziara yake ya kampeni, Mheshimiwa Doyo alisema ni aibu kwa wananchi wa Serengeti kuendelea kukosa barabara za uhakika, licha ya kuwa wilaya hiyo ni miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa za kiuchumi na kijamii.
Alisema baadhi ya mikoa ya Kaskazini imefaidika na uwekezaji mkubwa katika barabara na miundombinu ya usafirishaji, hali iliyorahisisha biashara na kuongeza kipato cha wananchi, tofauti na hali ilivyo Serengeti.
“Ni jukumu letu kuhakikisha Serengeti inakuwa na miundombinu ya kisasa. Tutajenga barabara za kiwango cha juu, ikiwemo barabara ya Zenge, sambamba na miradi mingine muhimu itakayorahisisha usafiri na kufungua fursa za maendeleo,” alisema Doyo.
Aidha, aliahidi kuunganisha Serengeti na Bunda, Arusha na maeneo mengine makuu ya kibiashara, ili kuongeza tija kijamii na kukuza uchumi endelevu wa wananchi.
“Ilani ya NLD imewaangalia kwa makini wananchi wa Mkoa wa Mara na Watanzania kwa ujumla. Serikali yetu itahakikisha barabara na miundombinu inakuwa nyenzo ya maendeleo ya wote,” aliongeza.
Baada ya mkutano huo, msafara wa mgombea huyo uliendelea kuelekea mkoani Mara, ambako anatarajiwa kuanza rasmi kampeni katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.





