TASINIA YA FILAMU KUNUFAIKA NA MAFUNZO YA FILAMU KUTOKA KOREA
Na Neema Mpaka - Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Rajabu Amiry, amerejea nchini akitokea Korea Kusini ambako alihudhuria mafunzo na mazoezi mbalimbali yanayohusiana na sekta ya filamu, akifuatana na timu kutoka Wizara husika, Bodi ya Filamu na Shirikisho la Filamu Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo 20 Septemba 2025, Rajabu alisema kupitia safari hiyo wamejifunza mambo mengi muhimu kuhusu sera, mafunzo na mazoezi ya filamu. Amesisitiza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuboresha tasnia ya filamu nchini.
“Hakuna siku tuliyopata nafasi ya kupumzika, mpaka siku ya Jumapili tulikuwa tunafundishwa na kufanya mazoezi mbalimbali. Lengo lilikuwa kupata mafunzo, siyo kutembea ama starehe,” alisema Rajabu.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Serikali ya Korea kupitia Shirika la KOICA kwa kuhakikisha Bodi ya Filamu inapata mafunzo hayo. Pia ameiomba Serikali ya Tanzania kuyaleta mafunzo hayo nchini ili wasanii wengi wapate nafasi ya kujifunza sera za filamu za Korea, ambazo zimeisaidia nchi hiyo kuwa na mfumo bora wa filamu.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, amesema katika mafunzo hayo wamekubaliana mambo mengi yatakayosaidia kuendeleza filamu nchini. Amewataka wadau wa filamu kutumia fursa hizo ili kuhakikisha zinachangia kwa vitendo maendeleo ya tasnia hiyo.





