Breaking News

PROF. KITILA AFUNGUA MAGAYE POLYCLINIC, AWAITA WANANCHI KUPATA HUDUMA

Dar es Salaam – Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ubungo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Profesa Kitila Mkumbo, amewataka wananchi kujitokeza kupata huduma za afya katika Magaye Polyclinic iliyopo Manzese Argentina, jijini Dar es Salaam.

Prof. Kitila alitoa wito huo mara baada ya kuzindua kituo hicho cha afya, akiwa katika kampeni zake za kuomba kura kwa wananchi wa Jimbo la Ubungo. Alipongeza jitihada za vijana kuwekeza katika sekta muhimu ya afya, akisema serikali imekuwa mstari wa mbele kuboresha na kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.
“Nimefarijika kuona uwekezaji huu mkubwa katika afya. Nichukue nafasi hii kuwapongeza kwa kufungua kituo hiki kitakachosaidia wakazi wa maeneo haya kupata huduma bora za afya,” alisema Prof. Kitila.

Baada ya uzinduzi huo, Prof. Kitila aliendelea na kampeni zake za nyumba kwa nyumba na mtaa kwa mtaa katika Kata ya Makurumla, akiwa ameambatana na Mgombea Udiwani wa CCM katika kata hiyo, Bakari Kimwanga.
Katika mikutano hiyo, walinadi ilani ya chama, wakieleza yaliyotekelezwa, kuchukua changamoto za wananchi, na kutoa ahadi za utekelezaji wa mahitaji yao endapo watachaguliwa tena kuongoza katika kipindi cha mwaka 2025–2030.