DOYO AZURU BUTIAMA, AAHIDI KUENZI MCHANGO WA BABA WA TAIFA, ASISITIZA AMANI, UMOJA NA MSHIKAMANO, KUPIGA VITA UDINI NA UKABILA
Butiama, Mara – Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, amefanya ziara maalum katika kijiji cha Butiama, mkoani Mara, ambako alizuru kaburi la Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Akiwa Butiama, Mhe. Doyo alisisitiza umuhimu wa kuenzi mchango wa Baba wa Taifa, akibainisha kuwa fikra na maono ya Mwalimu Nyerere ndiyo msingi wa kudumisha amani, mshikamano wa kitaifa na mapambano dhidi ya ukabila na udini.
“Taifa litaendelea kuwa imara iwapo tutadumisha misingi ya umoja, upendo na mshikamano aliyoacha Mwalimu,” alisema Mhe. Doyo.
Aidha, alieleza kuwa sera ya Uzalendo, Haki na Maendeleo ya chama chake imetokana moja kwa moja na falsafa za Mwalimu Nyerere. Alibainisha kuwa Ilani ya Uchaguzi ya NLD imejengwa juu ya tunu hizo kwa lengo la kumuenzi Nyerere na kuendeleza urithi wake wa kisiasa na kijamii.
Katika hotuba yake, Mhe. Doyo aliahidi kupunguza maslahi ya wabunge iwapo atachaguliwa kuwa Rais, akisema hatua hiyo itaonyesha dhati ya kuendeleza maono ya Mwalimu Nyerere aliyepigania siasa safi, usawa na uwajibikaji wa viongozi wa umma.
Alitumia fursa hiyo pia kuwataka Watanzania kuungana bila kujali tofauti za kikabila, kidini au kisiasa, akisisitiza kuwa amani, mshikamano na uzalendo ndizo nguzo kuu za maendeleo ya taifa.
Msafara wa mgombea huyo wa NLD unaendelea na kampeni zake mkoani Mara, na kesho unatarajiwa kufanya mikutano katika Wilaya ya Bunda.




