Breaking News

KONGAMANO LA KITAIFA LA WADAU WA UCHUMI WA BULUU LAANZA RASMI DAR ES SALAAM

Dar es Salaam, Septemba 10, 2025 – Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Uchumi wa Buluu limeanza leo katika Hoteli ya King Jada, Morocco Square jijini Dar es Salaam, na linatarajiwa kufanyika kwa siku mbili mfululizo hadi kesho, Septemba 11, 2025.

Mgeni rasmi, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Mitawi, amesema Serikali imedhamiria kutumia ipasavyo rasilimali za bahari na maji ya ndani kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

“Uchumi wa buluu ni injini mpya ya maendeleo ya Tanzania. Ukitumiwa kwa ufanisi unaweza kuongeza ajira, kukuza biashara na kuimarisha ustawi wa wananchi,” amesema Mitawi.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchukuzi, Mhandisi Shomari Shomari, amesema maboresho ya miundombinu ya bandari, reli na vyombo vya usafiri majini ni nguzo muhimu za kukuza uchumi wa buluu na kuongeza ushindani wa biashara kitaifa na kimataifa. Ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana ili kuhakikisha miradi ya usafirishaji inaleta manufaa kwa Taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Prof. Tumaini Gurumo, amesema chuo hicho kina jukumu la kutoa elimu, kufanya tafiti na kuzalisha wataalamu wanaohitajika katika sekta za bahari, usafirishaji na uhifadhi wa mazingira ya pwani.
“DMI ni nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa buluu kwa kuwaandaa vijana kushiriki kikamilifu kwenye sekta hii,” amesema Prof. Gurumo.

Kongamano hili limeandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Uchukuzi kupitia DMI, na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi – Zanzibar, likiwa na lengo la kuunganisha wadau na kuweka mikakati ya kitaifa ya kuendeleza uchumi wa buluu kwa njia endelevu.