USALAMA WAIMALISHWA JIJINI DAR KUELEKEA SIKUKUU YA MAULID
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limesema kuwa hali ya usalama kwa ujumla ni shwari na shughuli mbalimbali za kijamii na kisiasa zinaendelea kwa amani.
Akizungumza na waandishi wa habari, leo Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, SACP Muliro Jumanne Muliro, amesema jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuzuia uhalifu na kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani.
Tarehe 11 Agosti 2025, Polisi walimkamata mtuhumiwa Ramadhan Makala, mkazi wa Tabata, kwa tuhuma za kusafirisha magunia 13 ya bhangi yenye uzito wa kilo 239. Magunia hayo yalikuwa yamechanganywa na mchele yakisafirishwa kwa lori aina ya Fuso lenye usajili T.733 AGT kutoka Morogoro kuelekea Dar es Salaam.
Kuanzia tarehe 12 hadi 20 Agosti 2025, eneo la Magomeni Kinondoni, Polisi walikamata watuhumiwa wawili; Hassan Hamis mkazi wa Tandale na Elia Mapunda mkazi wa Goba, wakiwa na pikipiki sita zenye usajili tofauti pamoja na vipuli mbalimbali vinavyodaiwa kuwa vya wizi. Aidha, watuhumiwa wengine watatu waliokamatwa kwa makosa ya uvunjaji ni Gift Shabani (Kimara), Hussein Ally (Tandale) na Razaki Ramadhani (Manzese) ambapo walikutwa na televisheni 21 na simu 10 za wizi.
Kamanda Muliro alisema kuanzia tarehe 16 hadi 25 Agosti 2025, Jeshi la Polisi lilifanya msako na kukamata magari 15 yaliyokuwa yakitembea kwa namba za usajili zisizo rasmi za SSH 2530, kinyume na Sheria ya Usalama Barabarani.
Katika hatua nyingine, Polisi walieleza kuhusu mafanikio ya mashauri yaliyofikishwa mahakamani ambapo wahalifu mbalimbali walihukumiwa vifungo vikubwa kutokana na makosa ya ubakaji, kulawiti na unyang’anyi wa kutumia silaha. Aliyetajwa ni pamoja na Ashiri Bashiru Selemani (Kivule), Jumanne Onesmo Ngalya (Chanika), Tyson Fidel Malingumu (Chanika), Nicolaus Gabriel Thomas (Tabata Barakuda), Shafii Abdallah @Shado (Karakata), Samwel Kedymo @Sampepe (Kibamba) na Maulid Rashid @Mfuko (Mbezi).
Aidha, Polisi wametoa wito kwa wananchi hususan wazazi na walezi kuwa na uangalizi wa karibu kwa watoto wakati wa matembezi ya Sikukuu ya Maulid, huku wakisisitiza umuhimu wa kufuata sheria za barabarani ili kuepusha ajali.
“Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha waumini na wananchi wote wa Dar es Salaam wanasherehekea Sikukuu ya Maulid kwa amani na utulivu,” amesema SACP Muliro.