POLISI WATOA TAHADHARI KUELEKEA MICHEZO YA KIMATAIFA YA SOKA JIJINI DAR
Na Neema Mpaka - Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa tahadhari kuelekea michezo ya soka ya kimataifa itakayofanyika wiki hii jijini Dar es Salaam, likisisitiza kuwa maandalizi ya ulinzi na usalama yameimarishwa ili kuhakikisha mechi hizo zinachezwa kwa amani na utulivu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, jiji hilo linaendelea kuwa shwari huku mifumo ya kuzuia vitendo vya kihalifu ikiendelea kuimarishwa kwa ushirikiano na vyombo vingine vya dola.
Timu ya Yanga SC itashuka dimbani tarehe 25 Oktoba 2025 saa 11:00 jioni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Silver Strikers ya Malawi, huku Simba SC ikitarajiwa kucheza dhidi ya Nsingizini FC ya Eswatini tarehe 26 Oktoba 2025 saa 10:00 jioni.
Jeshi la Polisi limewakumbusha mashabiki na wapenzi wa soka kuwa silaha za aina yoyote hazitaruhusiwa kuingizwa uwanjani, na kwamba vitendo vya vurugu, uchochezi au uvunjifu wa amani havitavumiliwa. Aidha, magari yasiyo na kadi maalum za kuingia uwanjani hayataruhusiwa kuingia katika maeneo ya michezo.
Polisi wamewataka wadau wote wa soka kufuata taratibu na miongozo iliyowekwa, wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani kabla, wakati na baada ya michezo hiyo.
Aidha Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limezitakia mafanikio mema timu zote mbili za Tanzania.




