Breaking News

WAZIRI KOMBO AFUNGUA MKUTANO MKUU MAALUM WA TCCIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amezindua Mkutano Mkuu Maalum wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) ambapo amesisitiza umuhimu wa taasisi hiyo kuwa injini kuu ya diplomasia ya uchumi nchini.
 
Amesema kuwa licha ya mchango wake mkubwa katika kukuza biashara, TCCIA imepoteza fursa nyingi muhimu za kimataifa, hivyo ni wakati wa kujipanga upya ili kuwa daraja madhubuti kati ya sekta binafsi na Serikali katika kuvutia uwekezaji, masoko na teknolojia.
Akitoa hotuba yake, Waziri Kombo ameitaka TCCIA kuwa mshauri wa Serikali katika biashara za kimataifa, kuongoza safari za wafanyabiashara kwenda nje ya nchi, kutoa taarifa sahihi za masoko ya kimataifa, pamoja na kusaidia katika kuwaletea wawekezaji wa kigeni taarifa na mazingira rafiki ya kuwekeza nchini.

Amesema Wizara yake itaendelea kushirikiana kwa karibu a TCCIA kupitia jukwaa la diplomasia ya uchumi ili kuinganisha taasisi hiyo na majukwaa ya kimataifa ya biashara na wekezaji.
Ameipongeza TCCIA kwa hatua ya kuboresha Katiba yake na kuwataka viongozi wake kuimarisha nafasi ya taasisi hiyo katika utendaji wa diplomasia ya uchumi, akibainisha kuwa sekta binafsi ndiyo injini kuu ya kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Waziri Kombo ameahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na TCCIA katika utekelezaji wa mikakati ya kukuza uchumi kwa kutumia diplomasia ya uchumi
Kwa upande wake, Rais wa TCCIA, Bw. Vicent Minja, amesema kuwa mkutano huo umejikita katika kupitia na kuboresha katiba ya chemba hiyo ili iendane na mahitaji na mabadiliko ya sasa. 

Ameeleza pia kuwa mchakato huo unalenga kuhakikisha ushiriki mpana na jumuishi, hususan kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya TCCIA.