Breaking News

WANAHARAKATI HURU KUFANYA ZIARA YA KITAIFA MIKOA 15 KUHAMASISHA AMANI

Dar es salaam - Wanaharakati huru nchini wametangaza mpango wa kufanya ziara ya kitaifa itakayozunguka mikoa 15, kwa lengo la kuzungumza na vijana wa Kitanzania kuhusu umuhimu wa kudumisha amani na kushiriki katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza leo Januari 4, 2026, Mwanaharakati Huru, Kombo Ahmed Kombo, amesema kufanikisha ziara hiyo kunahitaji ushirikiano wa Watanzania wote, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo ya nchi.

Amesema katika kuhakikisha tunafanikisha ili wanaharakati hao wameomba kukutana na Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Vijana ili kufanya mazungumzo ya kina kuhusu masuala yanayowahusu vijana na namna bora ya kuyatatua.

Akizungumzia hotuba ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, iliyohusu uchaguzi uliomalizika, Kombo amesema Heche hana haki ya kuzungumzia uchaguzi ambao chama chake hakushiriki.

“CHADEMA waliamua kujitoa kwenye uchaguzi, hivyo kinachowafanya wazungumzie uchaguzi ambao hawakushiriki hakihusiani nao,” amesema Kombo.

Aidha, Kombo ameonya kuhusu makundi yanayodaiwa kupanga kufanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na taswira ya nchi, akiitaka Serikali kuwa makini na kufuatilia kwa karibu taarifa zinazojitokeza au kuandikwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Naiomba Serikali iwe macho na ichukue tahadhari mapema, kwani baadhi ya makundi haya hayana nia njema kwa nchi yetu,” ameongeza.

Katika hatua nyingine, Kombo ameupongeza uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa utekelezaji wa miradi na hatua mbalimbali za maendeleo, sambamba na kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya kulinda amani na usalama.

Amewahimiza vijana kutojiingiza katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi, akipinga kauli zinazodaiwa kuwahamasisha vijana kufanya vitendo visivyofaa.

Kwa upande wake, Joseph Yona maarufu 'Yona wa Chalinze' amesema kuna haja ya Watanzania kupongezana kwa kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini. Amesema ziara yao inalenga pia kutoa elimu kwa vijana kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo matumizi sahihi ya mikopo inayotolewa kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi.

Yona amewaomba wanahabari kujitokeza kuomba mikopo kupitia halmashauri zao badala ya, kwa kauli yake, “kuchochea migawanyiko” katika taifa lililojengwa kwa misingi ya umoja na amani na waasisi wa nchi.

Akizungumzia suala la maridhiano, Yona amesema maridhiano yanayozungumzwa siyo ya vyama vya siasa bali ni kati ya Watanzania na watawala, akieleza kuwa taasisi na makundi mbalimbali yatahusishwa katika mchakato huo.

Kuhusu madai ya utekaji, Yona amedai kuwa CHADEMA wanahusika katika baadhi ya matukio hayo na baadaye kuilaumu Serikali, akimwomba Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kuweka wazi ripoti ya matukio ya utekaji kwa kuwa, kwa mujibu wake, taarifa hizo zipo.

Ziara hiyo ya wanaharakati huru inatarajiwa kuanza hivi karibuni, huku ratiba kamili ya mikoa itakayohusishwa ikitarajiwa kutangazwa baadaye.