Breaking News

VYAMA 12 VYAIPONGEZA RIPOTI YA TUME YA JAJI CHANDE, VYAUNGA MKONO HOTUBA YA RAIS SAMIA

Dar es salaam - Vyama 12 vya siasa nchini vimepongeza ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya tarehe 29 na baada ya Uchaguzi Mkuu, iliyowasilishwa na Jaji Othman Chande, vikieleza kuwa imeweka msingi mzuri wa kuimarisha hali ya kisiasa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 26, 2026 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya vyama hivyo, Mheshimiwa Doyo alianza kwa kupongeza hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kufuatia kukubali mapendekezo yote yaliyotolewa na tume hiyo.

Mheshimiwa Doyo alisema hatua ya Rais kukubaliana na mapendekezo hayo inaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kutafuta suluhu ya kudumu ya changamoto za kisiasa zilizojitokeza wakati na baada ya uchaguzi.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa mamlaka husika kuyafanyia kazi kwa haraka pendekezo namba nne na la tano, akieleza kuwa utekelezaji wake utasaidia kuondoa mivutano ya kisiasa inayoendelea nchini.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Doyo alitaka hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote waliotajwa katika ripoti hiyo kuwa chanzo cha viashiria vya ghasia, ili kuhakikisha uwajibikaji na kudumisha amani na utulivu wa nchi.

Vyama hivyo vimehitimisha kwa kutoa wito kwa wadau wote wa kisiasa kushirikiana katika kutekeleza mapendekezo ya tume hiyo kwa manufaa ya taifa.