NLD YAWATAKIA WATANZANIA HERI YA PASAKA, YAHIMIZA UPENDO NA UMOJA WA KITAIFA
Chama cha NLD kimetoa salamu za heri ya Sikukuu ya Pasaka kwa Watanzania wote, kikisisitiza umuhimu wa kuendeleza tunu za kijamii na kiimani katika kipindi hiki muhimu.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Idara ya Habari na Mahusiano ya Umma ya chama hicho, NLD imewakumbusha wananchi kuenzi misingi ya upendo, mshikamano, uvumilivu na kusameheana, ikieleza kuwa maadili hayo ni nguzo muhimu katika kudumisha amani na kuleta maendeleo ya taifa.
Chama hicho kimeeleza kuwa Pasaka ni fursa adhimu kwa kila Mtanzania kujitafakari, kurekebisha mahusiano yaliyovunjika, na kuimarisha umoja wa kitaifa. Aidha, kimehimiza jamii kutumia kipindi hiki kujenga upya mshikamano na kuendeleza maadili mema yanayochochea ustawi wa pamoja.
Katika ujumbe huo, NLD pia imetoa wito kwa wananchi kuendelea kulinda amani, kuheshimiana, na kushirikiana katika juhudi za kujenga Tanzania bora kwa kizazi cha sasa na kijacho.
“Kwa pamoja, tuienzi Pasaka kwa matendo mema yanayoakisi utu na kujali wengine,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hii umetolewa na Mhe. Pogora Ibrahim Pogora kwa niaba ya Idara ya Habari na Mahusiano ya Umma NLD Taifa.




