WATANZANIA WAHIMIZWA KUDUMISHA AMANI KATIKA MAADHIMISHO YA PASAKA
Dar es salaam - Watanzania wameaswa kudumisha amani na mshikamano wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka, wakitakiwa kuupokea ufufuko wa Yesu Kristo kwa roho na kweli.
Wito huo umetolewa na Askofu wa Kanisa la WRC (The Word of Reconciliation Church), Askofu Nicklous Siguye, alipokuwa akitoa salamu za Pasaka kwa waumini na Watanzania kwa ujumla.
Amesema kuwa Watanzania wana utamaduni wa upole, upendo na kuthamini amani, hivyo ni muhimu kuendeleza tunu hizo hasa katika kipindi hiki cha kiimani.
Askofu Siguye amesisitiza umuhimu wa umoja wa kitaifa, akieleza kuwa wananchi wanapaswa kushikamana bila kujali tofauti za kidini, kisiasa au kikabila, ili kuijenga nchi yenye mshikamano na maendeleo endelevu.
Aidha, amewahimiza waumini kujiungamanisha zaidi na Yesu Kristo katika kipindi hiki muhimu cha kiroho kuanzia Ijumaa Kuu hadi Pasaka, wakitafakari juu ya mateso, kifo na ufufuko wake.
Katika hatua nyingine, Askofu Siguye ametangaza kuwa Jumatatu ya Pasaka itakuwa ni siku ya maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kanisa la WRC. Amechukua fursa hiyo kuwaalika Watanzania wote kushiriki katika maadhimisho hayo maalum yatakayohusisha ibada na kumtukuza Mungu kwa pamoja.
Amesisitiza kuwa maadhimisho hayo ni fursa ya kuimarisha imani, kuendeleza mshikamano na kuombea amani ya taifa.




