Breaking News

SERIKALI KUENDELEA KUIWEZESHA OSHA KUONGEZA UFANISI WA KAZI

Serikali imeahidi kuendelea kuiwezesha Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa kuipatia vitendea kazi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Deus Sangu, wakati akifunga maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Mjimwema, mkoani Njombe Region.

Waziri Sangu amesema OSHA ni taasisi muhimu katika kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi kwa ufanisi na katika mazingira salama, hivyo serikali ina wajibu wa kuiwezesha ipasavyo.

“Hivyo, serikali itaendelea kuipatia OSHA vitendea kazi vyote muhimu, ikiwemo magari na vifaa vya ukaguzi,” amesema Sangu.
Ameongeza kuwa hadi sasa serikali imeipatia OSHA magari 50 pamoja na vifaa vya ukaguzi vyenye thamani ya shilingi bilioni saba.
Katika maadhimisho hayo, Waziri Sangu pia aliziagiza OSHA, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) pamoja na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuhakikisha wanawabana waajiri kujisajili na kulipa michango pamoja na madeni wanayodaiwa.
Akizungumzia usajili wa OSHA, amesema licha ya kuwepo kwa takribani waajiri 200,000 nchini, waliokwisha fikiwa na OSHA hawazidi 100,000.

“Suala la kujisajili OSHA ni takwa la kisheria, si hiari. Kila mwajiri anapaswa kuhakikisha anajisajili,” amesisitiza.

Kwa upande wa WCF, Waziri Sangu amesema baadhi ya waajiri katika sekta binafsi bado hawajasajili wafanyakazi wao, na amewapa siku 90 kufanya hivyo kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amewahimiza wafanyakazi kutoa taarifa endapo hawataona mabango ya OSHA katika maeneo yao ya kazi.
“Katika maeneo yote yaliyosajiliwa, OSHA huweka mabango yao. Endapo hulioni bango hilo mahali pako pa kazi, toa taarifa ili hatua zichukuliwe,” amesema Nyamhokya.

Awali, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema kupitia maadhimisho hayo wamefanikiwa kuwafikia wajasiriamali 6,101 pamoja na maofisa usafirishaji 300 na kuwapatia vifaa kinga, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha usalama kazini.

Amesema OSHA itaendelea kutoa elimu, ushauri na uhamasishaji kuhusu afya na usalama mahali pa kazi, akibainisha kuwa hatua hizo zitasaidia kupunguza gharama kwa serikali pamoja na kuimarisha mifuko ya hifadhi ya jamii.