Breaking News

SHEIKH MCHAKA: ANAEYEDUKU KWA KUSEMA UKWELI NI SABABU YA KWENDA PEPONI

Waumini wa dini ya Kiislamu wamekumbushwa kushikamana na mambo sita ambayo Mtume Muhammad (SAW) aliwahakikishia kwamba wakidumu nayo watapata Pepo, likiwemo suala la kusema kweli.

Akitoa 'khutuba' ya Ijumaa katika Msikiti wa Jamiul Nurul Hikma, Temeke Mwembeyanga, mkoani Dar es Salaam, Sheikh Maulid Hussein Mchaka amesema hiyo ni ahadi kutoka kwa mbora wa viumbe, ambaye Qur'an inaeleza hasemi kwa matamanio yake binafsi, na ametumwa kuwa rehema kwa wanadamu.

"Pepo ni neema kubwa. Tunafundishwa kuwa hata mtu atakayepata pepo ndogo, ukubwa wake ni sawa na dunia hii mara kumi," amesema Sheikh Maulid, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ofisi ya Rais wa Al-Hikma Foundation, Sheikh Abdulqadir Al Ahdal, na Msimamizi Mkuu wa shughuli za ujenzi wa taasisi hiyo.

Sheikh Maulid amenukuu hadithi iliyopokewa na Ubadah ibn As-Samit kwamba Mtume alisema: "Niwekeni dhamana ya mambo sita kutoka kwenu, nami nitawadhaminia Pepo." Mambo hayo ni kusema kweli, kutimiza ahadi, kurudisha amana, kulinda tupu, kuinamisha macho dhidi ya haramu na kuzuia mikono isiwadhuru watu. Hata hivyo, Sheikh Maulid katika khutuba hiyo amejikita zaidi katika wosia wa kusema kweli, huku mengine akisema kila moja linahitaji khutuba nzima kufafanuliwa.

Amesema katika dunia ya sasa yenye maendeleo makubwa ya teknolojia, ilitarajiwa watu wawe wasema ukweli zaidi kwa kuwa njia za kujificha zimepungua, lakini hali imekuwa tofauti.

"Leo uongo umeshamiri. Watu wanatumia teknolojia kusema uongo. Mfano, mtu anatangaza bidhaa mitandaoni na kuisifu, lakini ukiinunua unakuta maelezo yote si ya kweli," amesema.

Aidha, amesema kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu, maneno yanayohukumiwa ni yale yanayotamkwa kwa ulimi, si yaliyofichwa moyoni. Amesema ulimi unaweza kuvunja ndoa, kugawa jamii na hata kuanzisha migogoro kati ya mataifa, lakini ukweli hujenga familia, huimarisha biashara, ujirani mwema na urafiki.

Sheikh Maulid pia amekumbusha hadithi nyingine inayohimiza waumini kujizoesha kusema kweli hadi waandikwe mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa ni "wasema kweli".

"Siku hizi ni nadra kumwonyesha mtu kwamba huyu ni mkweli wa mazungumzo. Mkweli yuko wapi? Tubadili tabia zetu," amesisitiza.