Breaking News

TFS YAWASUKUMA WANANCHI NA WANAFUNZI KUOKOA MISITU, VYANZO VYA MAJI

Na Mwandishi Wetu - Katika hatua inayodhihirisha dhamira ya serikali kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za asili, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Kituo cha Uzalishaji Mbegu za Miti, umetoa mafunzo maalum kwa wakazi wa Kata ya Mzinga pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Konga na Sekondari Konga, yakilenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda misitu na vyanzo vya maji.

Mafunzo hayo yaliyofanyika jana Aprili 25,2026 jijini Dar es Salaam, yameelezwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa TFS wa kuijengea jamii uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira, hususan katika kipindi hiki ambacho athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kuathiri upatikanaji wa maji na uhai wa misitu.

Kupitia mafunzo hayo, washiriki walipatiwa elimu ya kina kuhusu mbinu bora za upandaji miti, utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu, hatua inayolenga kuhakikisha kizazi cha sasa na kijacho kinanufaika na rasilimali hizo bila kuathiri mazingira.

Mafunzo hayo yalitekelezwa kwa ushirikiano wa wadau wa mazingira wakiwemo wataalamu kutoka Bodi ya Maji ya Bonde la Wami Ruvu na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), ambao walisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, taasisi na jamii katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Kituo TFS cha Uzalishaji Mbegu za Miti Morogoro, Mhifadhi Straton Chedelo alisema ni wakati sasa kwa jamii kubadili mtazamo na kuona uhifadhi wa mazingira kama jukumu la kila mmoja, badala ya kuiachia serikali pekee.

“Uhifadhi wa misitu na vyanzo vya maji si hiari, ni wajibu. Bila mazingira salama, hatuwezi kuwa na maisha bora wala maendeleo endelevu. Hivyo tunasisitiza ushiriki wa kila mwananchi,” alisema.

Aidha, aliwataka wanafunzi waliohudhuria mafunzo hayo kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii zao kwa kusambaza elimu waliyoipata, akieleza kuwa vijana ni nguzo muhimu katika kuhakikisha juhudi za uhifadhi zinaendelea kudumu kwa muda mrefu.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakiahidi kuitumia katika maisha yao ya kila siku pamoja na kuwahamasisha wenzao kushiriki katika shughuli za upandaji miti na utunzaji wa mazingira.

Hatua hiyo ya TFS inaendelea kuonesha mwelekeo wa taasisi hiyo katika kuhamasisha jamii kushiriki moja kwa moja katika uhifadhi wa misitu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kitaifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda vyanzo vya maji kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.