Breaking News

WAZAZI WAKUMBUSHWA JUKUMU LA KUJENGA VIJANA WENYE MAADILI NA UZALENDO

Na mwandishi wetu - Wazazi na walezi wametakiwa kutenga muda wa kuwa karibu na kuzungumza na vijana wao ili kuhakikisha wanapata malezi bora yenye maadili, sambamba na kutambua umuhimu wa amani, umoja na mshikamano uliopo nchini.

Wito huo umetolewa na wanawake wa Kanisa la Waadventista wa Sabato wakati wa semina iliyolenga kujadili namna ya kuwaandaa vijana kutambua na kuthamini tunu ya amani pamoja na kukabiliana na mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana wa kizazi cha sasa.

Baadhi ya washiriki wa semina hiyo, akiwemo Harris David, Debora Festus na Anna Anthony, wamesema wazazi wengi wa sasa wamekuwa na majukumu mengi, hali inayosababisha kushindwa kufuatilia kwa karibu mwenendo na tabia za vijana wao.

Wamesema hali hiyo huwanyima vijana malezi sahihi na ya karibu kutoka kwa wazazi wao kuhusu masuala muhimu ya kijamii na kitaifa, jambo linaloweza kuathiri mafungamano yao na jamii pamoja na kupunguza uzalendo wao kwa taifa.

Kwa upande wake, mwezeshaji wa semina hiyo, Sharifa Lauden, amesema wazazi na walezi wana wajibu mkubwa katika malezi na makuzi ya vijana ili kujenga taifa lenye vijana wazalendo na wenye maadili mema.

“Natoa rai kwa wazazi na walezi kuwalea watoto wao kwa kuwapa miongozo sahihi, hususan katika misingi ya kidini na maadili, ili kuwa na hofu ya Mungu na kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani pamoja na mmomonyoko wa maadili unaoendelea kujitokeza katika jamii,” amesema.