Breaking News

CHALAMILA ATOA MWEZI MMOJA KUONDOA VYUMA CHAKAVU BARABARANI, ASISITIZA ULINZI NA USAFI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa muda wa mwezi mmoja kwa wamiliki wa gereji na mafundi seremala kuondoa vyuma chakavu pamoja na samani chakavu zilizopo kandokando ya barabara, akisema hali hiyo imekuwa ikiharibu mwonekano wa jiji na kuathiri juhudi za kulifanya kuwa safi na la kuvutia.

Chalamila ametoa agizo hilo wakati akizungumza katika kikao kazi maalum kilichowakutanisha madiwani, wenyeviti wa mitaa, watendaji wa kata na mitaa pamoja na wakuu wa wilaya zote tano za Mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema viongozi wa ngazi mbalimbali wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kulinda usalama wa maeneo yao, ikiwemo kuanzisha vikundi vya sungusungu vitakavyosaidia kuimarisha ulinzi wa wananchi na mali zao.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam haitakuwa tayari kuona amani na utulivu wa mkoa huo vinavurugwa kwa namna yoyote, akieleza kuwa Dar es Salaam ni kitovu cha shughuli za kiuchumi na kidiplomasia nchini.

Akizungumzia taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu uwepo wa watu wanaopanga kufanya maandamano, Chalamila amewataka viongozi wa mitaa na kata kuendelea kusimamia amani katika maeneo yao na kuhakikisha hakuna vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa wananchi.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka viongozi wa serikali za mitaa kuimarisha usafi wa mazingira ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko. Amesema hatua hiyo ni muhimu hasa katika kipindi ambacho Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON), hivyo ni lazima kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na yenye kuvutia.

Ameelekeza wakurugenzi wa halmashauri kusimamia kikamilifu sheria na kanuni za usafi wa mazingira, kudhibiti utupaji taka ovyo na kuhakikisha wananchi wanapaka rangi majengo yao yaliyo kando ya barabara ili kuboresha mandhari ya jiji.
Kuhusu usimamizi wa taka, Chalamila amesema mchakato wa uendeshaji wa Dampo la Pugu Kinyamwezi kwa mfumo wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi unapaswa kuanza kabla ya Julai 30 mwaka huu. Pia amezitaka halmashauri zote kuwa na maeneo rasmi ya kutupia taka na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utenganishaji wa taka.

Vilevile, amepiga marufuku ubandikaji holela wa mabango na matangazo katika maeneo mbalimbali ya jiji na kuwataka wakurugenzi kutotoa vibali vya biashara za baa ndani ya maeneo ya makazi ya watu, hususan katika maeneo ya Masaki na Oysterbay.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Mhinte, amesisitiza matumizi sahihi ya anuani za makazi, akieleza kuwa mfumo huo utasaidia kutambua wakazi kwa urahisi na hivyo kuchangia kuimarisha usalama na amani katika jamii.