DKT. MWINYI AZINDUA AWAMU YA PILI YA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA WA MAMA SAMIA
Na. mwandishi wetu Zanzibar - Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezindua Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili (MSLAC II).
Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 20, Juni 2026 Katika Viwanja vya Dole Kizimbani Wilaya ya Magharibi “A” Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo Mhe. Dkt. Mwinyi amezitaka Wizara zote mbili zinazoshughulikia masuala ya sheria kuongeza ushirikiano na kubadilishana uzoefu ili kufanikisha kampeni hiyo.
“Kampeni ya Mswaada wa Kisheria ni nguzo muhimu ya kuimarisha Utawala bora, Upatikanaji wa haki na kichocheo cha amani, utatuzi wa migogoro, utulivu na ustawi wa jamii”, akifafanua umuhimu wa kampeni hiyo amesema Dkt. Mwinyi.
Aidha,Mhe. Dkt. Mwinyi kabla ya uzinduzi huo alikagua mabanda ya Maonesho ya Msaada wa Kisheria ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya kampeni hiyo na alipata fursa ya kutembelea banda la Idara ya Uhamiaji na kujionea huduma mbali mbali za Masuala ya kiuhamiaji zinazotolewa kwa Umma.
Mrakibu wa Uhamiaji Ame Mussa Maulid akimtolea ufafanuzi wa huduma za Uhamiaji Mhe, Rais amesema kuwa Idara ya uhamiaji kupitia maonesho hayo inatoa elimu kwa Umma juu ya huduma mbali mbali zinazotolewa na Uhamiaji Kwa Manufaa ya Taifa.
Akiongeza amesema kuwa wananchi katika Banda la Uhamiaji watapata elimu ya namna ya kuomba pasipoti ya kusafiria, vibali vya ukaazi, viza, hati za dharua za safari pamoja na maombi ya uraia wa Tanzania.
Kauli mbiu ya Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inasema “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo”.










