RC CHALAMILA: AMANI NA UTULIVU NI MSINGI WA SHUGHULI ZA KIBIASHARA NA KIUCHUMI
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amefungua kikao cha Baraza la Biashara la Mkoa wa Dar es Salaam na kuwataka wafanyabiashara pamoja na wananchi kwa ujumla kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi mkuu wa shughuli zote za kibiashara na kiuchumi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Four Points by Sheraton, Chalamila amesema kuwa bila kuwepo kwa amani na utulivu, shughuli za biashara na uwekezaji haziwezi kufanyika kwa ufanisi.
Ametaja mambo matatu muhimu yanayowezesha ukuaji wa uchumi na biashara kuwa ni amani, utulivu na uwepo wa sera bora za biashara zinazoweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na wafanyabiashara.
Aidha, RC Chalamila ameeleza kuwa bado kuna changamoto zinazohitaji nguvu ya pamoja ili kuendelea kuimarisha sekta ya biashara mkoani humo. Miongoni mwa changamoto hizo ni msongamano wa magari jijini Dar es Salaam pamoja na masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo ya biashara, hususan Kariakoo.
Amesema Serikali ya Mkoa inaendelea na jitihada za kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa Smart City kwa kuweka kamera za usalama zitakazosaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi na wafanyabiashara.
Pia, amebainisha kuwa changamoto nyingine ni ukosefu wa utamaduni wa kulipa kodi kwa baadhi ya Watanzania. Amehimiza umuhimu wa kujenga utamaduni huo kuanzia ngazi za chini za jamii, akieleza kuwa kodi ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa na uboreshaji wa huduma za kijamii.
Sambamba na hilo, amezitaka taasisi za serikali ikiwemo TRA, TBS na halmashauri kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuwalinda na kuwawezesha wafanyabiashara. Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kujipanga mapema ili kunufaika na fursa za kiuchumi zitakazotokana na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Yusuph Yenga, ameshauri vibali vya ujenzi vitolewe kwa wakati, hususan kwa miradi ya uwekezaji, ili wafanyabiashara waweze kunufaika kikamilifu na fursa zitakazotokana na AFCON 2027.
Yenga pia ameshauri kuimarishwa kwa biashara ya usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi na kueleza changamoto inayowakabili baadhi ya wafanyabiashara ya kutakiwa kuwasilisha risiti za mauzo kabla ya kuuza bidhaa wanazosafirisha nje ya nchi.
Akifafanua suala hilo, Mwakilishi wa Mikoa Mitano ya Kikodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dar es Salaam, Festus Patta, amesema kuwa katika utaratibu wa usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi (export), mfanyabiashara anatakiwa kuwa na nyaraka za mauzo ikiwemo invoice, ambazo hutumika kuthibitisha thamani ya bidhaa zinazouzwa.
Aidha, ameahidi kuwa TRA itaendelea kufanyia kazi changamoto hiyo ili kuhakikisha wafanyabiashara wanapata huduma bora na mazingira rafiki ya kufanya biashara.












