MTANDAO YA KIJAMII ITUMIKE KUJENGA TAIFA, SI KUCHOCHEA VURUGU
Vijana nchini wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ya maendeleo binafsi na ya taifa badala ya kuigeuza kuwa chombo cha kueneza chuki, uchochezi na taarifa zinazoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Wito huo umetolewa wakati viongozi mbalimbali, taasisi na wananchi wakiendelea kusisitiza umuhimu wa kudumisha utulivu kuelekea Julai 7, 2026, kufuatia taarifa za kuwapo kwa wito wa maandamano unaosambazwa kupitia mitandao ya kijamii.
Akizungumza na waandishi wa habari, mkazi wa Chanika, Dar es Salaam, Bw. Jonas Mdodo, amesema mitandao ya kijamii ni fursa muhimu kwa vijana kujifunza, kufanya biashara na kujiongezea kipato, lakini baadhi ya watu wamekuwa wakiitumia vibaya kwa kuhamasisha vurugu na kusambaza taarifa za taharuki.
"Mitandao ya kijamii ni fursa muhimu, lakini kuna wanaoitumia kufanya uchochezi, kuhamasisha vurugu na kueneza taarifa za taharuki. Nawashauri vijana wenzangu kuitumia kwa njia zinazotuinufaisha na kuchangia maendeleo ya taifa badala ya kutuvuruga," amesema Mdodo.
Aidha, amewataka vijana wanaofikiria kushiriki maandamano kuzingatia athari zilizojitokeza katika matukio ya Oktoba 29, 2025, na kuweka mbele maslahi ya taifa.
Kwa upande wake, Bw. Baraka Rwegoshora amesema vijana wanapaswa kuungana kuwalinda wenzao dhidi ya ushawishi wa watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi. Amesisitiza kuwa mabadiliko ya kisiasa yanapaswa kufanyika kupitia njia halali na za kikatiba, ikiwemo uchaguzi.
Katika siku za hivi karibuni, viongozi wa serikali, viongozi wa dini, vyama vya siasa na wananchi wameendelea kutoa wito wa kulinda amani na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha machafuko. Wamesisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku wakionya dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii katika kuhamasisha vitendo vinavyokiuka sheria.




