MHE. NAPE NNAUYE AILIPUA SERIKALI BUNGENI

Mbunge Nape Nnauye amefunguka na kuibana serikali ya awamu ya tano kupitia Waziri wake Mkuu kuwa kitendo cha hotuba yake Bungeni kutokuwa na hata neno moja linalohusu gesi ni usaliti mkubwa kwa wananchi wa Lindi na Mtwara kwa kudai gesi ndiyo yalikuwa makubaliano yao wakati wa kupiga kura.
Nape
ametoa kauli hiyo leo Aprili 09, 2018 Bungeni katika mkutano wa 11 kikao cha
tano cha Bunge la 11 linaloendelea kufanyika Mjini Dodoma baada ya kuipitia
hotuba ya Waziri Mkuu ambayo inatakiwa kusomwa mbele ya Wabunge huku ikiwa
haina hata neno moja kuanzia mwanzo wa ukurasa hadi mwisho linaloshabiana na
gesi na mafuta.
"Tulipopiga
kura mwaka 2015, tuliamini kwamba uchumi wa gesi kwa mikoa ya Lindi na Mtwara
ni ukombozi mkubwa na upo salama mikononi mwa Rais Magufuli na serikali ya
awamu ya tano. Tulipopiga kura ndio ukawa mkataba wetu siyo kwa maneno, kwa
hiyo kura alizozipata Rais Magufuli ni kwa sababu ya makubaliano yaliyopo ndani
ya ilani ya uchaguzi ya CCM ambapo ndani yake kuna masuala ya gesi kwamba
atakwenda kuyaendeleza", amesema Nape.
Pamoja na
hayo, Nape ameendelea kwa kusema "hivi ni bahati mbaya kwamba hotuba ya
Waziri Mkuu imeshindwa kuliona jambo hili kuwa ni kubwa na ikaamua kuliacha au
serikali imeamua kuachana nalo kwa sababu naona jitihada kubwa zinaenda kwenye
umeme wa maji lakini umeme wa maji katika ilani haumo. Ilani tumezungumza
nishati ya gesi tena kwa sehemu kubwa sana. Hii ndio ilikuwa imani ya wanalindi
na mtwara kwa serikali ya awamu ya tano".
Aidha,
Nape amesema wakati mchakato wa kupata madini hayo katika mkoa wa Lindi na
Mtwara wananchi wengi walipoteza maisha yao huku wengine wakipata ulemavu na
majeraha mbalimbali ili mradi kuiwezesha nchi yao iwe na nishati ya gesi na
mafuta.
"Kuna mali za watu zilipotea lakini tukaamini
kuna neema kesho yake. Jambo hili bahati mbaya tulimkabidhi sisi Rais Magufuli
tukaamini lipo salama, alipotupa Majaliwa tukaamini tupo salama zaidi kwa
sababu Waziri Mkuu ametoka kwetu. Sasa ni bahati mbaya sana kwamba humu ndani
hakuna kabisa neno gesi maana yake ni kwamba hili jambo limeanza kuachwa sasa
ili tuende kwenye umeme wa maji. Lakini je hatusaliti Ilani ya uchaguzi CCM
pamoja na wananchi wa Lindi na Mtwara waliotupa kura na kutuamini kwamba gesi na
uchumi wao upo salama?", amehoji Nape.
Nape
ameendelea kusisitizia
"Hili ni bomu kubwa, wakati wa mchakato hali
ya kisiasa, kijamii Lindi kulikuwepo na tabu sasa imetulia tukiamini neema ipo
lakini kiuchumi baada ya harakati za gesi na mafuta kusini watu walianza
kuekeza na uchumi ulikuwa, ila hali ya sasa waekezaji wanaondoka na uchumi
umeanza kudorola, hali yetu ngumu sana".
Kwa
upande mwingine, Nape amemuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa asikubali suala la
gesi lisiwe mikono mwake yeye akiwa Waziri Mkuu wa Tanzania.



