Breaking News

AWAMU YA PILI KUWAHAMISHA WANANCHI NGORONGORO KUKAMILIKA MACHI 2024

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo bwana Mobhare Matinyi akifafanua jambo katika mkutano wake na waandishi wa habari (hawapo pichani) uliofanyika 3 december 2023 katika chuo cha Utalii jijini Dar es Salaam.

Dar es salaam:
Serikali imesema awamu ya Pili ya kuwahamisha wananchi kwa hiari kutoka katika hifadhi ya Ngorongoro kuelekea Msomera Wilayani Handeni mkoani Tanga lililoanza Julai mwaka huu linatarajiwa kukamilika Machi 2024.

Akizungumza jijini Dar es salaam juu ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika zoezi la kuwahamisha wananchi wa Ngorongoro Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, bwana Mobhare Matinyi amesema awamu ya kwanza serikali ilijenga nyumba 503 ambapo Kaya 551 zilihamia kwa hiari zikiwa na jumla ya watu 3010 pamoja na mifugo 2521.

"Katika eneo hili na Msomera, ili wananchi wahamie kwa hiari Serikali ilifanya mambo mawaili. Moja ilitoa elimu kwa wananchi, kwanini imefika wakati wa kuwahamisha Ngorongoro na kuwapeleka kwenye maeneo waliyowatengea. Na jambo lingine la msingi sana ni Serikali kuhakikisha kuwa inalinda haki za watu hawa na kuwapa vitu vitakavyowashawishi na kuwasaidia katika maeneo hayo," Alisema Bw. Matinyi. 

Alisema kila Kaya iliyokubali kwa hiari kwenda Msomera inajengewa na kupewa nyumba bure nyenye vyumba vitatu vya kulala. Eneo la ekali mbili, hati miliki ya eneo lake, pamoja na kupewa eneo la ekari tano na hati miliki, iwapo ana mifugo sambamba na kutengewa eneo kwa ajili ya malisho ya mifugo.

Aidha bwana Matinyi aliongeza kuwa katika awamu hii ya pili iliyoanza Julai mwaka huu serikali imeweka lengo la kujenga nyumba 5000 katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wananchi wa hao ikiwemo eneo la Msomera.

Alisema nyumba hizo 5000 zitakapo kamilika zinatarajiwa kupokea Kaya ambazo zitakubali kuhama kwa hiari kutoka Ngorongoro, Serikali hamzuii mtu aliyepo Ngorongoro kuhamia kwa hiari yake kwenye maeneo mengine ya Nchi pamoja na Wamasai kutawanyika katika mikoa takribani 14 ya Tanzania, lakini serikali ilichukua pori Tengefu la Handeni (Msomera) na kulitenga kwa ajili yao.