TEA - VIJANA 49,000 WANUFAIKA NA MRADI WA KUENDELEZA UJUZI
Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi (TEA) Bwana Masozi Nyirenda akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) namna taasisi hiyo inavyoteleza majukumu yake katika maonesho ya miaka 50 ya Baraza la Mtihani la Tanzania yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam viwanja vya Mnazi Mmoja.
Kaimu Mkurugenzi Huduma za Taasisi Mwanahamisi Chambega akiongea na waadishi wa habari juu ya ushiriki wa taasisi ya elimu katika katika maonesho ya miaka 50 ya Baraza la Mtihani la Tanzania yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam viwanja vya Mnazi Mmoja.
Dar es Salaam:
Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania nchini (TEA) imefanikiwa kukamilisha mradi wa kuendeleza ujuzi kwa mafanikio makubwa ambapo jumla ya vijana 49,000 wamenufaika kwa kupata ujuzi nchini.
Akizungumza katika maonyesho ya miaka 50 ya baraza la mtihani (NECTA) Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi (TEA) Bwana Masozi Nyirenda amesema Katika kufanikisha utekelezaji wa malengo haya, Serikali imeendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta ya Elimu kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari hadi vyuo vikuu.
"Serikali imeendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta ya Elimu kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari hadi vyuo vikuu. Maboresho na mageuzi haya yanahitaji rasilimali na nguvu kazi kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha sekta ya sekta ya Elimu nchini." Alisema Bw. Nyirenda.
Alisema Mamlaka ya Elimu Tanzania pia inalo jukumu la kuhamasisha uchangiaji maendeleo ya Elimu kote nchini ambapo, kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Elimu, Namba 8 ya mwaka 2001 sehemu ya 12 (1) (a) na (b) mchangiaji ni mtu yeyote anayetoa mchango wa pesa, bidhaa, au huduma kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa au kutekeleza mradi kwa uratibu wa Mfuko huo wa Elimu.
Aidha bwana Nyirenda alibainisha kuwa mchangiaji anaweza kuwa mtu yeyote anayetoa udhamini au ruzuku kwa wanafunzi mbali na watoto wake, familia yake au mwajiri wake, kwa lengo la kuwasaidia kuendelea na elimu kwenye ngazi ya sekondari au elimu ya juu ambapo udhamini huo atautoa kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa.
"Napenda kutoa wito kwa Wadau na wachangiaji wa maendeleo ya Elimu kote nchini kutoa michango yao kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa ili waweze kutangazwa na kutambuliwa kitaifa, ambapo mchangiaji huandikwa katika rejesta ya kudumu ya wachangiaji wa elimu" Alisema Bw. Nyirenda.
Akizungumzia ushiriki wa taasisi hiyo katika maonesho ya baraza la mitihani Tanzania, Bwana Nyirenda amesema wao kama wadau wakubwa wa elimu nchini hivyo ni muhimu wakakutana na wananchi na kutoa elimu juu ya kazi wanazozifanya.
“Wenzetu baraza la mtihani (NECTA) wanatathimini ubora wa elimu, sisi tunafadhili vifaa na kuhakikisha mazingira ya ufundishaji yanakuwa bora, kwa hiyo tupo hapa kueleza fursa zinazopatikana,” alisema Bw. Nyirenda
Alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza, na kusimamia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ikiwemo kusimamia upatikanaji wa elimu bora na kwa usawa kote nchini pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia.






