Breaking News

WARIOBA, KIKWETE NA KINANA WAMMWAGIA SIFA ALHAJI ALI MWINYI

Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi akitoa heshima zake za mwisho mbele ya jeneza la Hayati Mwinyi
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akitoa heshima zake za mwisho mbele ya jeneza la Hayati Mwinyi
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza kwenye katika ibada ya kitaifa ya kumuaga hayati Mwinyi

Mama Sitti Mwinyi akitoa heshima zake za mwisho mbele ya jeneza la Hayati Mwinyi
Bi Khadija Mwinyi (Mjane wa marehemu) akitoa heshima zake mbele ya jeneza la Hayati Mwinyi

Na mwandishi wetu
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Hayati Alhaji Ali Hassan Mwinyi alikua Kiongozi asiyejikwaza,alikua mtu mwenye mapenzi na watu wote.

Kikwete amesema hayo leo Machi mosi alipozungumza na viongozi mbalimbali pamoja na waombolezaji waliohudhuria hafla ya kumuaga kitaifa Hayati Mwinyi kwenye Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

"Mwinyi aliishi maisha ya kawaida ya uungwana ,alikua msikivu na alikua ni mtu wa kupokea maoni na zaidi ya yote alinifundisha kuwa na maamuzi hasa kwenye vitu vyenye maslahi ya taifa yeye ndiye baba wa mageuzi ya uchumi na kisiasa hapa nchini" Amesema Rais Mstaafu Kikwete.

Naye Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa awamu ya pili Mstaafu Joseph Warioba akimzungumzia Hayati Mwinyi amesema kuwa "Leo ni siku ya majonzi ya kyondokewa na mzee Mwinyi lakini pia ni siku ya furaha ya kusherehekea maisha yake kwa mengi aliyoyafanya wakati alipolitumikia taifa hili, kwani amekuwa na juhudi nyingi za kuleta maendeleo hasa kwenye nyanja ya kiuchumi na kisiasa" Amesema Warioba. 

Wakati huohuo Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana amemuelezea Hayati Mwinyi kwa kusema kuwa "Sote ni mashahidi kwamba Hayati Ali Mwinyi alifanya jitihada za kuitoa nchi ya Tanzania kwenye mfumo wa chama kimoja kwenda kwenye mfumo wa vyama vingi" amesema Kinana.

Ameongeza kwa kusema kuwa suala hili halikuwa rahisi vilevile alitupeleka kwenye uchumi huria alifanya yote haya mengine mengi huku akimshirikisha Hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa lengo la kuhakikisha kwamba mabadiliko yanafanyika kwa utulivu na kulinda amani na utulivu wa nchi.

Kabla ya kupelekwa Uwanja wa Uhuru mwili wa Alhaji Mwinyi umeswaliwa katika msikiti wa BAKWATA na maziko yatafanyika kesho Zanzibar.