MHE. ZAIDAT FUNDI: TUILINDE AMANI, TUDUMISHE MAADILI YA KISIASA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU
Zanzibar – Mwenyekiti wa Kigoda cha Wanawake Taifa wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Mhe. Zaidat Fundi, ametoa wito kwa Watanzania kulinda amani ya taifa na kudumisha maadili ya kisiasa, hasa kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za chama hicho zilizopo Uwanja wa Ndege Zanzibar, Mhe. Zaidat alielezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la lugha za matusi na kejeli, hasa dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia mitandao ya kijamii.
“Watanzania na Wanaafrika Mashariki wanapaswa kuelewa kuwa Rais wa Tanzania ni mwanamke. Kumkosoa mwanamke kunahitaji staha, utu na nidhamu. Hatupingi ukosoaji, lakini tujiulize: tunamkosoaje? Ukosoaji usiwe jukwaa la kumdhalilisha mtu mwenye hadhi ya mzazi wako,” alisisitiza Mhe. Zaidat.
Katika hotuba yake, alitoa rai kwa vyombo vya usalama kuhakikisha kunakuwa na mazingira salama kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Alieleza kuwa amani ni msingi wa maendeleo ya taifa lolote, na hivyo ni lazima ihifadhiwe kwa nguvu zote.
Mhe. Zaidat pia alipendekeza Tume Huru ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi kuandaa makongamano ya kitaifa kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu haki, mipaka na wajibu wao katika kipindi cha uchaguzi.
"Watanzania wanapaswa kupewa elimu ya kutosha kuhusu madhara ya uchochezi mitandaoni na kuelewa uzito wa kesi zinazohusiana na uchochezi. Tunahitaji uchaguzi wa amani, unaozingatia sheria, maadili na utu," aliongeza.
Akihitimisha, Mhe. Zaidat alisema kuwa uongozi bora hujengwa katika msingi wa maadili, nidhamu, elimu ya kiraia, pamoja na ushiriki wa haki na uwajibikaji wa kila mwananchi katika mchakato wa kidemokrasia na kisiasa.

.jpg)


