Breaking News

PROFESA ANNA TIBAIJUKA: "PESA HAZITOKANI NA SERIKALI, CHANZO NI WANANCHI"

Dar es Salaam – Mwanasiasa mkongwe nchini, Profesa Anna Tibaijuka, amesema kuwa fedha za maendeleo hazitokani moja kwa moja na Serikali, bali zinatokana na wananchi ambao ndio chanzo kikuu cha rasilimali za taifa.

Akiwasilisha mchango wake katika kongamano la Kitaifa kuhusu ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), lililofanyika mkoani Dar es Salaam, Profesa Tibaijuka alisisitiza kuwa mfumo wa PPP ni nguzo muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Amesema kuwa kupitia mfumo huu, uwazi huimarishwa na wananchi wanashirikishwa moja kwa moja katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hatua inayojenga uwajibikaji na ushirikiano wa kweli kati ya Serikali na sekta binafsi.

"PPP siyo tu njia ya kuimarisha uchumi, bali ni utamaduni wa kushirikiana kwa uwazi, jambo linalowezesha miradi mikubwa kujadiliwa bungeni na kupewa kipaumbele," amesema Profesa Tibaijuka.

Awali, mada kuu ya kongamano hilo iliwasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila, ambaye alieleza umuhimu wa ushirikiano huo katika kuchochea maendeleo ya kitaifa.

Kongamano hilo limewakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi kwa lengo la kujadili njia bora za kushirikiana katika kuleta maendeleo endelevu nchini.