Breaking News

RAIS WA NAMIBIA AHUTUBIA UDSM, AWASHAURI WANAWAKE KUJIKITA KWENYE MALENGO YAO

Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, akitoa mhadhara maalum katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mei 21, 2025.
Mkuu wa Chuo, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akitoa mhadhara maalum katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mei 21, 2025.


Dar es Salaam – Wanawake nchini na duniani kote wamehimizwa kujielekeza katika malengo waliyojiwekea na kutokubali kuathiriwa na jitihada zozote, hata kama zinatoka kwa watu wa karibu, zitakazowapotosha au kuwakwamisha.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, wakati akitoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Mei 21, 2025.

Mhadhara huo uliobeba kichwa cha habari "Kuwahamasisha Wanawake Kuvunja Vizuizi vya Kuelekea Nafasi za Uongozi" (Inspiring Women to Break the Barriers in Leadership Positions), uligusia historia ndefu ya harakati za kuwawezesha wanawake, ikiwemo madai ya haki ya kupiga na kupigiwa kura, umiliki wa mali, na ushiriki wa kisiasa na kijamii.
Rais Nandi-Ndaitwah alisema kuwa usawa wa kijinsia ni jambo la msingi kwa maendeleo ya kweli, akirejea Mkutano wa Dunia wa Wanawake uliofanyika Beijing mwaka 1995, ambao alihudhuria kama mmoja wa wajumbe.

"Kufikia ulipokusudia kunahitaji msimamo thabiti na nidhamu ya hali ya juu. Wanawake tunapaswa kuzingatia hayo ili kutimiza malengo yetu," alisema.

Aidha, aliwataka wanawake kuchukulia changamoto za dunia ya sasa kama fursa za kujifunza na sio sababu ya kurudi nyuma. Alieleza kuwa mateso ya ukoloni, ikiwemo yeye kufungwa na kuikimbia nchi, hayakumzuia bali yalimsukuma kufikia mafanikio.
Akihitimisha, alisema kuwa wanawake wa leo wanaishi katika jamii yenye elimu na ujuzi wa hali ya juu, tofauti na miaka iliyopita, hivyo hakuna kisingizio cha kutofikia malengo yao.

Kwa upande wao, viongozi wa UDSM wakiongozwa na Mkuu wa Chuo hicho, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, walieleza kufarijika na heshima waliyopewa na Rais Nandi-Ndaitwah na kusema mhadhara huo utabaki kuwa kumbukumbu ya kihistoria kwa chuo hicho.