Breaking News

SEKTA YA MADINI YAVUNJA RECORD CHINI YA UONGOZI WA RAIS SAMIA, UWEKEZAJI, AJIRA NA MAPATO YAPAA - WAZIRI MAVUNDE

Dar es Salaam, Mei 24, 2025 – Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameeleza mafanikio makubwa ya sekta ya madini nchini Tanzania katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika mkutano maalum na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba yake, Waziri Mavunde aligusia maeneo mbalimbali muhimu ambayo yamepiga hatua kubwa na kuonyesha mafanikio ya sekta hiyo kimkakati na kwa manufaa ya Watanzania.

1. Ongezeko la Bajeti

Bajeti ya Wizara ya Madini imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka – kutoka shilingi bilioni 89 (2023/2024) hadi shilingi bilioni 231 (2024/2025), huku mwaka 2025/2026 ikitarajiwa kuwa shilingi bilioni 224. Bajeti hii imeelekezwa zaidi kwenye Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa ajili ya tafiti na ujenzi wa maabara ya kisasa ya madini Dodoma, na nyingine mikoa ya Geita na Mbeya.

2. Mchango wa Sekta kwenye Pato la Taifa (GDP)

Sekta ya madini imefikisha mchango wa asilimia 10.1 kwenye GDP ifikapo Desemba 2024, ikiwa ni mafanikio makubwa kwa kuwa lengo hilo lilipangwa kufikiwa mwaka 2025.

3. Mpango wa Mining Vision 2030

Kupitia kaulimbiu ya “Madini ni Maisha na Utajiri”, mpango huu unalenga kuongeza kiwango cha tafiti za madini kutoka asilimia 16 hadi 50 ifikapo 2030. Sekta imechangia mzunguko wa fedha wa takribani trilioni 1.7 na mauzo ya nje ya madini kufikia asilimia 56.2 ya mauzo yote nje ya nchi.
4. Maduhuli Yameongezeka

Makusanyo ya maduhuli kutoka sekta ya madini yameongezeka kutoka shilingi bilioni 162 (2015/2016) hadi shilingi bilioni 753 (2023/2024). Kwa mwaka huu wa fedha (2024/2025), tayari bilioni 930 zimekusanywa hadi Mei 24, huku lengo likiwa ni trilioni 1.

5. BoT Yaingia Rasmi Kwenye Ununuzi wa Dhahabu

Sheria mpya ya Madini ya mwaka 2024 imeruhusu BoT kununua asilimia 20 ya dhahabu inayozalishwa nchini. Tangu Oktoba 2024 hadi sasa, tani 3.7 za dhahabu zimenunuliwa.

6. Uwezeshwaji kwa Wachimbaji Wadogo

Wachimbaji wadogo sasa wanachangia asilimia 40 ya mapato ya sekta. Serikali imefuta leseni 2,648 ili kuwawezesha kupata maeneo ya uchimbaji. STAMICO imewanunulia mashine za kuchoronga miamba na Serikali inahamasisha taasisi za fedha kuwapa mikopo.

7. Viwanda vya Uongezaji Thamani

Eneo la mgodi wa zamani wa Buzwagi limebadilishwa kuwa eneo la viwanda, ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha kusafisha makinikia cha Tembo Nickel Refining Limited, kwa lengo la kuongeza thamani ya madini na ajira nchini.

8. Minada ya Vito

Minada ya madini ya vito kama Tanzanite imerejeshwa, ikiwa ni juhudi za kuongeza thamani na kutangaza madini ya kipekee ya Tanzania kimataifa.
9. Marekebisho ya Sheria

Sheria mpya inabainisha kuwa leseni za uchimbaji mdogo ni kwa ajili ya Watanzania pekee, huku wageni wakiruhusiwa kushiriki kwa masharti maalum, hatua ambayo imepunguza migogoro kati ya wachimbaji na wawekezaji.

10. Miradi Mikubwa ya Madini

Serikali inaendelea kusimamia miradi mikubwa ya uchimbaji ikiwemo mradi wa Nyanzaga (Sengerema) na kuvutia wawekezaji wa kimataifa.

11. STAMICO Yaimarika

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeongeza mapato yake kutoka bilioni 1 hadi bilioni 84 ndani ya miaka minne. Limejitegemea kifedha na lina mpango wa kuanzisha kampuni tanzu ya miradi mikubwa.

12. Ajira kwa Watanzania na Local Content

Asilimia 97 ya ajira katika sekta ya madini ni kwa Watanzania, huku zaidi ya 19,000 wakiwa wameajiriwa moja kwa moja. Watanzania pia wanatoa huduma muhimu migodini.

13. Madini Mkakati

Serikali iko mbioni kukamilisha mkakati wa kuyavuna madini mkakati kama graphite, nickel na rare earths kwa maslahi ya taifa.

14. Programu ya MBT – Mining for a Brighter Tomorrow

Mpango huu unalenga kuwawezesha vijana na wanawake kwa kuwapatia leseni na maeneo ya uchimbaji. Tayari zaidi ya leseni 2000 zimetolewa Nyamongo, Mara.

15. Vituo vya Ukodishaji Mitambo

Vituo vya ukodishaji mitambo ya kisasa vimeanzishwa kusaidia wachimbaji wadogo kuongeza tija.

16. Sarafu za Dhahabu (Gold Coins)

Serikali iko kwenye mazungumzo na BoT kuanzisha sarafu za dhahabu kwa ajili ya akiba na malipo, ikiwa ni hatua ya kuwawezesha wananchi kuwekeza kwenye dhahabu.

17. Vikao na Wawekezaji

Serikali inaendelea kufanya vikao vya wazi na wawekezaji ili kubaini na kutatua changamoto zao kwa wakati.

18. Masoko ya Madini

Masoko 43 ya madini na vituo 109 vya ununuzi vimeanzishwa nchi nzima kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata masoko ya uhakika na kudhibiti utoroshaji.

19. Ushirikiano wa Kimataifa

Wizara ya Madini imesaini mikataba ya ushirikiano na nchi kama Uingereza, Sweden na Finland kwa lengo la kupata ujuzi, teknolojia na mitaji.

Hitimisho Waziri Mavunde amesisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya uongozi thabiti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na dhamira ya Serikali ya kuifanya sekta ya madini kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa nchi, viwanda na ustawi wa wananchi.