VIJANA UCHUMI CHALLENGE 2026: RAIS SAMIA KUTUNUKU WASHINDI JULAI 5 JNICC
Dar es salaam - Serikali imesema imejipanga kuhakikisha mawazo yote ya ubunifu yaliyowasilishwa na vijana katika shindano la kitaifa la Vijana Uchumi Challenge 2026 hayabaki kwenye makaratasi, bali yanaunganishwa na fursa za uwekezaji, taasisi za fedha na wadau wa maendeleo ili yawe miradi na biashara zenye kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa maendeleo ya vijana Joel Nanauka wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya hafla ya utoaji wa tuzo kwa washindi wa shindano hilo.
Amesema hafla hiyo itafanyika Julai 5, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, kuanzia saa mbili asubuhi, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Waziri huyo alisema shindano hilo limeandaliwa kwa lengo la kuwapa vijana nafasi ya kutumia ubunifu, maarifa na vipaji vyao katika kutafuta suluhisho za changamoto za kiuchumi na kijamii, kuongeza ajira, kuimarisha uzalishaji na kukuza ujasiriamali.
Alisema serikali inaamini vijana ni nguvu muhimu katika maendeleo ya taifa, hivyo imeanzisha mfumo wa kutambua, kukuza na kuwawezesha vijana wenye mawazo bunifu kwa kuwaunganisha na wawekezaji, taasisi za kifedha na wadau mbalimbali wa maendeleo.
"Hatutaki mawazo ya vijana yaishie kuwa maandishi ya miradi.Tunataka yawe biashara, huduma na miradi itakayogusa maisha ya wananchi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi," alisema Mhe. Nananuka
Alieleza kuwa shindano la mwaka huu lilikuwa na kaulimbiu isemayo "Vijana Tunafikiri, Taifa Linasonga," ikiwa ni ujumbe unaosisitiza umuhimu wa kuwashirikisha vijana katika kutafuta suluhisho za maendeleo ya taifa.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kampeni ya uhamasishaji ilifanyika kuanzia Aprili 13 hadi Mei 7, 2026 kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, vyuo na taasisi mbalimbali nchini.
Alisema jumla ya mawazo 7,892 yalipokelewa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo baada ya mchakato wa uchambuzi washiriki 100 walichaguliwa na kupelekwa katika kambi maalumu ya mafunzo iliyofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
Katika kambi hiyo, washiriki walipatiwa mafunzo kuhusu elimu ya fedha, ujasiriamali, ubunifu, uandishi wa miradi, namna ya kuwasilisha mawazo mbele ya wawekezaji na majaji pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu na wafanyabiashara waliofanikiwa.
Baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo, washiriki 10 bora walichaguliwa kuingia hatua ya fainali, ambapo watashindana mbele ya Rais Samia katika hafla ya Julai 5.
Waziri huyo alisema mchakato mzima wa shindano umeendeshwa kwa uwazi na weledi kupitia Kamati ya Taifa ya Vijana Uchumi Challenge pamoja na jopo la majaji wabobezi kutoka sekta mbalimbali.
Aliwapongeza wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Joseph Malekela, pamoja na majaji kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kuhakikisha washindi wanapatikana kwa haki na kwa kuzingatia ubora wa mawazo.
Aidha, alisisitiza kuwa si washindi watatu pekee watakaonufaika na programu hiyo, bali washiriki wote 100 wataendelea kuunganishwa na fursa mbalimbali za uwekezaji, ufadhili na ushauri wa kitaalamu ili mawazo yao yaweze kutekelezwa.
Aliongeza kuwa hafla hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, mabalozi, taasisi za fedha, sekta binafsi, wadau wa maendeleo, vijana kutoka Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na vyombo vya habari.
Waziri huyo aliwataka Watanzania, hususan vijana, kufuatilia tukio hilo, akieleza kuwa linafungua ukurasa mpya wa kuwawezesha vijana kutumia ubunifu wao kama nyenzo ya kukuza uchumi wa taifa.




