Breaking News

THABO MBEKI: MUSTAKABALI WA AFRIKA UPO MKONONI MWA WAAFRIKA WENYEWE

Rais mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mheshimiwa Thabo Mbeki, akitoa hotuba katika mhadhara maalum wa Siku ya Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Rais mstaafu wa Awamu ya Nne na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwasilisha mada katika mhadhara wa Siku ya Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah, UDSM.
Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Thabo Mbeki, akihudhuria mhadhara wa Siku ya Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Dar es salaam - Rais mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mheshimiwa Thabo Mbeki, ameshiriki katika mhadhara maalum wa Siku ya Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akihutubia katika mhadhara huo, Mhe. Mbeki amesema maadhimisho ya Siku ya Afrika yamelenga kuwakutanisha wasomi, vijana na Taasisi ya Thabo Mbeki ili kujadili kwa pamoja hatua za kuchukuliwa katika kuleta maendeleo ya bara la Afrika.

Akitumia muktadha wa kihistoria, Mhe. Mbeki alieleza hali ya sasa ya Afrika kuwa bado inakumbwa na athari za ukoloni, udhaifu wa taasisi za ndani, utegemezi mkubwa kwa mataifa ya nje, pamoja na changamoto ya Umoja wa Afrika na taasisi zake kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake.
"Kesho ya bara la Afrika haiwezi kuamuliwa na watu wengine, bali itategemea uamuzi, juhudi na mshikamano wa Waafrika wenyewe," alisisitiza Mhe. Mbeki.

Aidha, alieleza kuwa pamoja na mafanikio ya kisiasa yaliyopatikana baada ya uhuru, bado Afrika inakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi, kiusalama, na ukosefu wa mshikamano wa bara.

Mhe. Mbeki amezisihi nchi za Afrika kuhakikisha kuwa umoja na mshikamano vinaendelezwa, huku akisisitiza kuwa taasisi za Umoja wa Afrika na Tume ya AU zitekeleze majukumu yao kwa mujibu wa misingi ya kuanzishwa kwao.
Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuwa na viongozi wa kisiasa wenye maono kama hayati Mwalimu Julius Nyerere, akisema kuwa viongozi wa aina hiyo ndio wanaohitajika kuliongoza bara la Afrika kuelekea maendeleo ya kweli.

Katika hitimisho la hotuba yake, Mhe. Mbeki alitoa wito kwa vijana wa vyuo vikuu kushirikiana na wenzao kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, kutumia nafasi walizonazo kutoa mwelekeo wa nini kifanyike kufufua matumaini na mustakabali wa bara la Afrika.



Rais mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mheshimiwa Thabo Mbeki, akisalimiana na viongozi mbalimbali alipowasili katika Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).