WAZIRI JAFO ATOA WITO KWA WASANII KUSAJILI ALAMA ZA BIASHARA NA KAZI ZA SANAA
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo akimkabidhi Tuzo mmoja wa washindi katika maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani 2025, yaliyoandaliwa na BRELA na kufanyika katika hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani 2025, yaliyoandaliwa na BRELA na kufanyika katika hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, akitoa ufafanuzi katika maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani 2025 yaliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam, chini ya uratibu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
Afisa Mtendaji Mkuu wa COSOTA, Bw. Philemon Kilaka, akitoa hotuba wakati wa maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani 2025, yaliyoandaliwa na BRELA katika hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Dar es salaam - Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amewataka wasanii nchini kusajili alama za biashara kama vile nembo za bendi na studio ili kulinda kazi zao dhidi ya uharamia na kuhakikisha wanapata manufaa ya kiuchumi kupitia bunifu zao.
Dkt. Jafo ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani 2025, yaliyoratibiwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), ambapo pia tuzo zilitolewa kwa wabunifu waliofanya vizuri katika kusajili kazi zao.
“Alama zenu za biashara zinaweza kusajiliwa kupitia BRELA, hivyo kupata umiliki wa kipekee utakao wawezesha kuzitumia sokoni na kuepuka kufanyiwa uharamia,” alisema Jafo.
Aidha, amewasihi wasanii kusajili kazi zao kupitia COSOTA ili kuhakikisha wanapata mirabaha wanaponyimwa ridhaa ya kazi zao kutumika na watu wengine.
Waziri Jafo amesema usajili huo utawawezesha wasanii kuwa na kipato cha uhakika na kuongeza ubora wa kazi zao. Amesisitiza kuwa kwa nafasi yake kama Waziri mwenye dhamana ya miliki bunifu, ataendelea kushirikiana na taasisi kama BRELA na COSOTA kulinda haki za wabunifu nchini.
“Ninawasihi tuungane katika kusikilizia mdundo wa miliki bunifu, tuwalinde wasanii wetu ili wafaidike na kazi zao si tu nchini bali hata kimataifa,” aliongeza.
Katika tukio hilo, Dkt. Jafo aliwapongeza washindi wa Tuzo za Taifa za Miliki Ubunifu (NIPA) 2025 na kuwataka kutumia tuzo hizo kama motisha ya kuendeleza bunifu zaidi na kuzilinda kisheria.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, amesema licha ya mafanikio ya muziki wa Tanzania kuvuka mipaka ya kimataifa, bado kuna changamoto ya wasanii kutosajili kazi zao, hali inayowanyima fursa ya kunufaika na kazi zao kisheria.
“Muziki si burudani tu, ni biashara. Na biashara yoyote inalindwa. Wasanii wengi wanapoteza mapato kwa sababu kazi zao hazijasajiliwa,” alisema Nyaisa.
Ameongeza kuwa BRELA itaendelea kutoa elimu na huduma kwa wasanii ili kuhakikisha wanatambua umuhimu wa kulinda kazi zao kupitia miliki bunifu.
Kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho hayo ni “Muziki na Miliki Bunifu Tanzania: Sikiliza Mdundo wa Miliki Bunifu.”
Nyaisa amehitimisha kwa kuahidi kuwa BRELA itaendelea kushirikiana na COSOTA kuhakikisha kazi za ubunifu nchini zinalindwa na kuwa chanzo imara cha kipato kwa wabunifu na wasanii.













