Breaking News

WAZIRI MASAUNI AUNGANA NA UJUMBE WA WAZIRI MKUU JAPAN MAONYESHO YA DUNIA YA EXPO 2025

Japan - Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Masauni ameungana na ujumbe wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, katika ziara yao nchini Japan kushiriki Maonesho ya Dunia ya EXPO 2025 yanayofanyika Osaka, Japan.

Leo Mei 25, 2025, ikiwa ni Siku ya Taifa la Tanzania (Tanzania National Day) katika maonesho hayo, ujumbe wa Tanzania umeendelea kuonyesha utajiri wa nchi katika sekta mbalimbali zikiwemo utalii, uwekezaji, teknolojia na utamaduni.
Ushiriki wa Tanzania katika maonesho haya makubwa duniani unalenga kuitangaza nchi kimataifa, kuvutia wawekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa hususan katika sekta za maendeleo endelevu na mazingira.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayoshiriki kikamilifu katika EXPO 2025, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kukuza diplomasia ya uchumi na kulinda mazingira.