Breaking News

ACT WAZALENDO YAITAKA SERIKALI ISITISHE KUFUTWA KANISA LA GWAJIMA

Dar es Salaam — Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya za Kijamii, tarehe 02 Mei 2025, imetangaza rasmi kulifutia usajili Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima. Uamuzi huo unadaiwa kufuatia matamko ya hivi karibuni ya Askofu Gwajima aliyekemea vikali vitendo vya utekaji wa watu ambavyo vimekithiri nchini.

Mbali na hatua hiyo, baadhi ya waumini wa kanisa hilo wameripotiwa kukamatwa na polisi, hali inayoibua maswali kuhusu uhuru wa kuabudu na haki ya wananchi kukusanyika kwa amani.

Chama cha ACT Wazalendo kimejitokeza kulaani vikali hatua hiyo, kikieleza kuwa ni juhudi za serikali ya CCM kuzima sauti zinazokemea maovu na kukandamiza haki za msingi zilizowekwa na Katiba.

Katika taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa chama hicho, Bi. Shangwe Ayo, ACT Wazalendo wametoa wito kwa serikali kusitisha mara moja uamuzi huo, wakisema unakiuka uhuru wa maoni na uhuru wa kidini.

"Hatua ya kumvutia usajili Askofu Gwajima ni jaribio la kuzima sauti ya haki. Tunamuunga mkono kwa ujasiri wake wa kukemea utekaji unaoendelea nchini, licha ya hofu ya kushughulikiwa na vyombo vya dola," alisema Shangwe.

Chama hicho kimeitaka jamii ya Watanzania kuungana kukemea ukiukwaji wa haki za binadamu, hasa vitendo vya utekaji, kupotea kwa watu, na mauaji, vikisisitiza kuwa Tanzania haipaswi kugeuzwa kuwa kitovu cha utekaji.

ACT Wazalendo pia wametangaza kuendelea na msimamo wake wa kupambana na vitendo hivyo, wakihimiza wananchi kuichukulia hatua serikali ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao kwa kushindwa kulinda haki za binadamu na maisha ya wananchi.