Breaking News

MAAFISA 11 WA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI KANDA YA MASHARIKI WAPANDISHWA VYEO

Dar es Salaam – Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kanda ya Mashariki limewapandisha vyeo Maafisa 11 wa jeshi hilo waliokamilisha kozi mbalimbali za kitaaluma, hatua iliyolenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za zimamoto na uokoaji.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya zoezi la uvalishaji vyeo lililofanyika leo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, Naibu Kamishna wa Jeshi (DCF) Kennedy Komba amewapongeza maafisa hao huku akiwahimiza kufanya kazi kwa weledi na kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika majukumu yao ya kila siku.

"Leo tumefanya zoezi la uvalishaji vyeo kwa maafisa wa ngazi mbalimbali, ambao Mheshimiwa Rais ameridhia kupandishwa vyeo kwa mujibu wa taratibu za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji," alisema DCF Komba.
Aidha, alifafanua kuwa mchakato wa kupandishwa vyeo umezingatia utendaji kazi wa maafisa husika na kwamba hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Kwa mujibu wa DCF Komba, baadhi ya maafisa waliopandishwa vyeo wanatoka katika ngazi ya Kamishna Msaidizi (Assistant Commissioner) hadi Mkaguzi wa Zimamoto na Uokoaji. Amesema zoezi hilo awali lilipaswa kufanywa na Kamishna Jenerali mwenyewe lakini alikaimishwa kulitekeleza.

"Kwa niaba ya Kamishna Jenerali, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kibali alichotoa. Kupandishwa kwa maafisa hawa kutaongeza ari ya kufanya kazi na kuwapa nafasi ya kutekeleza majukumu mapya ya kiuongozi, hivyo kuchochea tija katika utoaji huduma kwa jamii," aliongeza
Alieleza pia kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani imekuwa na mchango mkubwa katika mchakato huo, na kwamba upandishwaji huo wa vyeo umetolewa kwa maafisa waliopo kwenye mikoa ya Lindi, Pwani na Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi mpya wa Jeshi hilo Tanzania Bara, ACF Chrispin Jackson Rabiuzima, ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Mkoa wa Ilala, aliishukuru serikali kwa kutambua mchango wao na kuahidi kuongeza bidii katika kazi.

"Tunaishukuru serikali kwa kutuamini na kutupandisha vyeo. Kwa hakika hii ni motisha kwa kila mmoja wetu. Tutaendelea kuchapa kazi kwa bidii na kuimarisha huduma kwa wananchi," alisema ACF Rabiuzima.
Kwa mujibu wa ACF Rabiuzima, maafisa waliopandishwa vyeo wametoka katika Kamandi za Zimamoto za Temeke, Ilala, Kinondoni, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mkoa wa Pwani, Mkoa wa Morogoro na Lindi.

Mgawanyo wa maafisa waliopandishwa vyeo ni kama ifuatavyo:

Kutoka Mrakibu Mwandamizi hadi Kamishna Msaidizi: 2

Kutoka Mrakibu hadi Mrakibu Mwandamizi: 4

Kutoka Mrakibu Msaidizi hadi Mrakibu: 3

Kutoka Mkaguzi Msaidizi hadi Mkaguzi: 2

Kwa ujumla, upandishaji huu wa vyeo unaonesha dhamira ya dhati ya serikali katika kuimarisha taasisi za ulinzi na usalama kwa kutambua mchango wa watumishi wake.